WANAFUNZI 6,862 KUFANYA MTIHANI WA KUHITIMU DARASA LA SABA 2019 WIKI IJAYO HALMASHAURI YA BUKOBA


Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Bukoba Mhe. Hashim Murshid Ngeze

Na Lydia Lugakila - Malunde1 blog Kagera
Halmashauri ya wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera imesema imekamilisha  kwa asilimia 98 maandalizi ya Mtihani kwa wahitimu wa darasa la saba 2019 unaotarajiwa kufanyika Septemba 11-12 Mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 7 2019, na Mwenyekiti wa Halmshauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera Mhe. Hashim Murshid Ngeze wakati akiongea na vyombo vya habari katika ofisi za halmashauri hiyo.

Mhe. Ngeze amesema Halmashauri hiyo ina shule 141 za kiserikali na 8 za binafsi huku akitaja jumla ya wanafunzi ambao wanatarajia kufanya mitihani wilayani humo kuwa wasichana ni 3511 na wavulana ni 3351 hivyo kufanya idadi ya wahitimu kuwa 6,862.

Mhe. Ngeze amesema hadi sasa Mitihani imeishawasili wilayani humo na zoezi la kuigawa kwenda shule za msingi ili kila shule iweze kuipata mitihani yake ambapo pia kiasi cha fedha kwa ajili ya kusimamia mitihani hiyo tayari imeletwa na bajeti ipo tayari akieleza kuwa maandalizi yamefikia asilimia 98.

Amesema anatarajia matokeo mazuri skwa kuwa hivi karibuni serikali imetoa pikipiki kwa waratibu wa elimu kata ili ufuatiliaji wa shule ya msingi uende vizuri na kwamba hata kwa upande wa mitihani ya ndani wa shule ya msingi kujipima wanafunzi walifanya vizuri kutokana na usimamizi mzuri.

"Wito wangu kwa wazazi na walezi wa watoto wanaotarajia kufanya Mtihani huo ni kuwa karibu na watoto kuwaliwaza,ili wasiwe na mawazo wakiwa ndani ya mtihani kwa sababu kushindwa kwa mtihani kunaanzia na maandalizi ya mtoto kutoka nyumbani anapoingia ndani ya chumba cha mtihani ana mawazo inasababisha kushindwa kufuata maelekezo ya mtihani’’,amesema

Amesema kuwa kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wazazi wanaowashinikiza watoto wao wasifanye vizuri kwenye mitihani yao ili kushindwa kuingia kidato cha kwanza kwa sababu ya umbali mrefu wa kufuata shule huku akitolea mfano shule ya msingi Kasharu na Rukoma kuwa hilo limekuwa likifanyika.

Ameongeza kuwa hivi karibuni alitembelea shule ya msingi Kamukore kati ya wanafunzi 19 wanafunzi 7 walikiri kwamba wazazi wao wameishawaambia wasifanye vizuri mtihani wao wa darasa la saba kwa sababu ya ukosefu wa shule ya sekondari hivyo  amewataka wazazi kutolipa kipaumbele suala hilo ili watoto wao wapate elimu sitahiki na kutimiza ndoto zao.

Amebainisha kuwa  zaidi ya shilingi milioni 600 zimepokelewa kutoka serikalini ili kuwezesha elimu bila malipo na kumshukuru Rais wa Jamhuli ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa kuanzisha utaratibu wa elimu bila malipo kwa sababu inaondolea wazazi mzigo wa kulalamika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post