Na Josephine Majura, Kondoa
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amemuagiza Kaimu Mhandisi wa Wilaya ya Kondoa, Felcitism Tesha kung’oa milango yote katika Kituo cha Afya Busi kutokana kutokuwa na viwango vya kuridhisha.
Ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya kikazi katika Kijiji cha Busi wilayani Kondoa kukagua utekelezaji wa miradi ya Ujenzi wa Vituo vya Afya vinavyojengwa kwa fedha za Serikali.
Dkt. Kijaji ambae pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini alisema kuwa hajaridhishwa na milango iliyowekwa katika kituo hicho kwa kuwa ubora wake hauendani na thamani ya fedha iliyotolewa kwa ajili ya utengenezaji wa milango hiyo.
Alisema fedha iliyotengwa kwa ajili ya milango hiyo ni kubwa zaidi ya milango inavyoonekana, hali inasababisha kuhatarisha usalama wa wagonjwa na watumishi wa kituo hicho.
“Nina agiza milango yote iliyowekwa ikiwa chini ya kiwango ibadilishwe kwa gharama za fundi aliyepewa tenda hiyo bila kutumia hata shilingi moja ya Serikali, milango haina hata mwaka imeanza kupasuka.”,alisisitiza Dkt. Kijaji.
Aidha, alitoa wito kwa Uongozi wa Wilaya kwa kushirikiana na Kamati ya Ujenzi ya Kijiji hicho kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kikamilifu katika kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ili kubaini mapungufu na kuyafanyia kazi mapema.
Aliongeza kuwa fedha zilizotolewa na Serikali ni nyingi hivyo lazima vifaa vinavyotumika katika ujenzi wa vituo hivyo viendane na thamani ya fedha hizo na Wananchi waone kazi nzuri na kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika Sekta ya Afya.
Naye Kaimu Mhandisi wa Wilaya ya Kondoa, Bw. Felcitism Tesha alimuahidi Dkt. Kijaji kwamba atatekeleza agizo hilo na kuhakikisha milango hiyo inabadilishwa kwa haraka kabla ya kuleta madhara kwa wagonjwa na watu wengine katika kituo hicho.
Kwa upande wake Mwanakijiji wa Busi, Bw. Hussein Ally, ameishukuru Serikali kwa juhudi mbalimbali inayofanya katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hasa huduma za jamii na kusifia huduma inayotolewa na watumishi wa Kituo cha Afya Busi.
MWISHO.
Social Plugin