Hatimaye ndege ya Serikali ya Tanzania iliyokuwa inashikiliwa nchini Afrika Kusini kwa amri ya Mahakama Kuu ya Gauteng, nchini humo imewasili Tanzania leo Jumatano Septemba 4, 2019 saa 2:25 usiku.
Ndege hiyo aina ya Airbus A220-300 ilizuiwa katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo tangu Agosti 23, 2019 imetua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kupokewa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi.
Akizungumza uwanjani hapo Profesa Kabudi amesema, “Kwetu ni jambo la furaha na shauku tumeweza kushinda kesi mahakamani na ndege imesharudi, tunawashukuru majaji wa Afrika Kusini kwa kutenda haki na hatimaye ndege imetua.”
Alipoulizwa kama kuna wasiwasi wowote juu ya ndege hiyo, Profesa Kabudi alijibu; “Kwa sasa hakuna wasiwasi wowote tena lakini tunaendelea kufuatilia hali halisi ili tuwe na uhakika kuwa hakuna wasiwasi tena. “Tunachukua tahadhari zote na tutahakikisha kuwa ndege zetu ziko salama.”
Chanzo - Mwananchi