Pakistan imesema imekataa ombi la Rais Ram Nath Kovind wa India la kutaka ndege yake kutumia anga yake wakati akielekea barani Ulaya huku mgogoro baina ya nchi hizo mbili jirani ukiendelea kutokota.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Shah Mehmood Qureishi alitoa taarifa siku ya Jumamosi na kusema, "rais wa India ameomba idhini ya kutumia anga ya Pakistan kuelekea Iceland lakini tumeamua kutomruhusu".
Amesema uamuzi huo wa Pakistan umechukuliwa kutokana na sera za hivi karibuni za India.
Pakistan ilizuia ndege zote za India kuruka katika anga yake baada ya ndege za kivita za nchi hizo mbili kukabiliana angani mwezi Februari mwaka huu.
Baadaye mwezi Julai Pakistan iliruhusu ndege za kiraia za India kutumia anga yake. Aghalabu ya ndege zinazoelekea au kutoka India hulazimika kutumia anga ya Pakistan na zisipofanya hivyo basi masafa ya safari huwa marefu sana.
Mwezi uliopita wa Agosti, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alibatilisha mamlaka ya kujitawala eneo la Kashmir hatua ambayo Pakistan iliitaja kuwa kinyume cha sheria.
Itafahamika kuwa, sehemu moja ya Kashmir iko chini ya udhibiti wa India na nyingine iko Pakistan. Nchi zote mbili zinadai kuwa wamiliki wa Kashmir yote.
Mgogoro wa Kashmir ulianza wakati Pakistan na India zilipotengana mwaka 1947 baada ya kuondoka mkoloni Muingereza.