Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAIPONGEZA KAMPUNI YA USAMBAZAJI YA ROUTE PRO KWA UWEZESHAJI VIJANA WA KUWAPATIA PIKIPIKI 30


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Ajira na Vijana ,Anthony Mavunde (kushoto) akimkabidhi pikipiki, Peter Mushi mkazi wa Makole Jijini Dodoma moja ya kampuni iliyotolewa na kampuni ya usambazaji ya Route Pro kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana kibiashara. 
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Ajira na Vijana ,Anthony Mavunde (kushoto) akijaribu kuendesha moja ya pikipiki zilizotolewa kwa ajili ya kuwezesha vijana na Kampuni ya Route Pro Katika hafla iliyofanyika Dodoma,kushoto ni Meneja Uendeshaji wa Kampuni hiyo Jaja Mbazila ,Kulia ni Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo,Duane Edward na nyuma ni baadhi ya vijana watakaonufaika na msaada huo 
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Ajira na Vijana ,Anthony Mavunde akimkabidhi Augustine Dotto moja ya pikipiki iliyotolewa na Kampuni ya Route Pro. 
Meneja Mkuu wa Kampuni ya usambazaji Bidhaa ya Route Pro akikabidhi funguo za pikipiki zilizotolewa kwa ajili ya kuwawezesha vijana kibiashara kwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Ajira na Vijana Anthony Mavunde wakati wa hafla hiyo iliyofanyika jijini Dodoma Katika viwanja vya Nyerere Square 
***
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana na Ajira),Antony Mavunde, ameipongeza kampuni ya kitanzania ya usambazaji bidhaa ya Route Pro kwa ubunifu wake utakaowezesha vijana kupata ajira ambapo imetoa pikipiki 30 kwa vijana kutoka mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Arusha, Moshi na Singida ambapo pia itawapatia mafunzo ya biashara.

Mavunde, alitoa pongezi hizo katika hafla ya kampuni ya Route Pro, kukabidhi pikipiki 10 kwa vijana wa mkoani Dodoma iliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini humo.

“Ukosefu wa ajira kwa vijana ni moja ya changamoto inayolikabili taifa letu, ili kukabiliana nalo Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele kushirikiana na wadau wanaonyesha nia ya kusaidia kubuni mipango endelevu ya kuwezesha ajira kwa vijana , kama ilivyofanya kampuni ya Route Pro, kwa kutoa mafunzo ya biashara kwa vijana wetu,Tutaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kufanikisha suala hili,” alisema Mavunde.

Kampuni ya Route Pro, itatoa pikipiki 30 kwa vijana sambamba na kuwapatia elimu ya biashara na usambazaji bidhaa pia itawapatia elimu ya kutumia vifaa vya teknolojia ya kisasa vya kusaidia kuratibu usambazaji na taarifa.Vijana hao pia itawaunganisha na wadau wake katika biashara na wazalishaji wengine na kushirikiana nao kusambaza bidhaa za wateja katika masoko mkakati ambao utawanufaisha vijana hao na kampuni kwa kugawana faida itakayopatikana nusu kwa nusu.

Akiongea katika zoezi la kuwachagua vijana hao, Meneja Uendeshaji wa kampuni ya Route Pro, Jaja Mbazila, alisema kampuni hiyo imepata walengwa wa kushirikiana nao katika mpango huu, kutokana na rekodi yake ya vijana ambao imewahi kufanya nao kazi katika miradi yake mbalimbali ya usambazaji bidhaa katika siku za nyuma na imewachagua waliokuwa wanafanya kazi kwa bidii na wenye malengo ya kukua kibiashara.

“Tumelenga kuwawezesha vijana wenye bidii ya kazi na kujituma kupata fursa kuwa na biashara zao,tumefanya nao kazi kwa karibu katika miaka iliyopita na wameonyesha kuwa na nia ya kufanya vizuri biashara ya usambazaji”,alisema Mbazila.

Aliongeza kuwa mbali na kuwapatia pikipiki,RoutePro itawapatia vijana hao kiasi cha shilingi 100,000/- kila mmoja ziwasaidie kuanzia kazi.

Baada ya miezi 24, pikipiki hizo zitakuwa mali yao kwa ajili ya kuwasaidia katika shughuli za usambazaji,ingawa watakaopenda kufanya kazi katika mpango huu wa Route Pro wa kuwezesha vijana watajiunga tena katika mpango wa miaka 2 na kupatiwa tena tena pikipiki mpya.

Route Pro ni kampuni ya Kitanzania yenye uzoefu mkubwa wa biashara ya usambazaji wa bidhaa,kwa hivi sasa inazo pikipiki zaidi ya 250 za usambazaji nchini kote,na inatumia teknolojia ya kisasa za kupata taarifa za mauzo kwa ajili ya kuzifanyia uchambuzi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com