Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

LUGOLA AAGIZA ASKARI WOTE WA KITUO CHA MAJIMOTO WAHAMISHWE.... WANANCHI WATAKA MKUU WA KITUO ABAKI


Na Adelina Ernest - Malunde 1 blog
Waziri wa mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola ametoa siku saba kwa Polisi Mkoa wa Katavi kuwahamisha askari wote wa kituo cha Polisi Majimoto kwa madai kushindwa kushugulikia kutatua kero za wananchi pamoja na kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Lugola alitoa agizo hilo jana jioni Jumapili Septemba 29, 2019 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika stendi ya Majimoto Halmashauri ya Mlele mkoani Katavi wakati akijibu kero za wananchi ambao walieleza kuwepo kwa kero lukuki katika kituo cha polisi Majimoto hali iliyomlazimu kuagiza askari wote 15 wa kituo hicho kuondolewa.

Waziri Lugola alisema kupitia kero zilizowasilishwa na wananchi, zinaonyesha wazi askari hao 15 wanajihusisha na rushwa, kupiga wananchi ovyo wakiwemo bodaboda, kushindwa kudhibiti ulinzi na usalama na kutoshughulikia malalamiko ya wananchi.

"Nataka niseme haya kutoa mfano, ili iwe fundisho kwa wengine kote nchini, Kaimu kamanda, natoa siku saba askari wote wa kituo hiki wahamishwe na waletwe wengine ili wajifunze," alisema Lugola.

Baada ya agizo hilo, Waziri Lugola aliwauliza wananchi askari wote wanatakiwa kuhamishwa? ambapo walipinga mkuu wa kituo hicho Iddy Kombo asihamishwe badala yake wahamishwe askari wengine wote.

"Asihamishwe, asihamishwe, asihamishwe," walisema wananchi.

Awali mmoja wa wananchi wa Majimoto Malugu Mayombi ambaye ni mkulima wa zao la Mpunga alieleza kero yake ya kutapeliwa Mpunga gunia 600 zenye thamani ya Sh.Milioni 60 na Mfanyabiashara anayejulikana kwa jina la Sali Kulwa maarufu kama TBS lakini jeshi la Polisi limeshindwa kumpa msaada.

Hata hivyo amewataka kutimiza wajibu wao kama Jeshi la Polisi na kuhakikisha hali ya usalama unaimarika katika kata hiyo kwani maendeleo huambatana na ulinzi na usalama wa kutosha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com