Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS MAGUFULI AONGEZA SIKU SABA WATUHUMIWA UHUJUMU UCHUMI KUTUBU


Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), Biswalo Mganga amesema ofisi yake imepokea barua za watuhumiwa 467 wanaoomba kukiri makosa ya uhujumu uchumi na wapo tayari kurudisha fedha jumla ya Shilingi 107.8 Bilioni.

Akiwasilisha taarifa yake leo Jumatatu Septemba 30, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, Mganga amesema watuhumiwa wameitikia wito alioutoa Rais John Magufuli

DPP amemuomba Rais Magufuli kuongeza siku tatu kwaajili ya kuwapa nafasi watuhumiwa wa uhujumu uchumi walio tayari kutubu na kurejesha fedha na mali ambao barua zao zimechelewa kufika ofisini kwake.

Akijibu ombi hilo, Rais Magufuli ametoa siku saba kuanzia leo Jumatatu Septemba 30, 2019 hadi Oktoba 6, 2019.


“Kama kweli wapo walikwamishwa na DPP umeniomba siku tatu mimi naona nikupe siku saba ili usije ukaniomba tena siku nyingine, nilitoa siku sita kwamba watuhumiwa wote wanaotaka kupata huu masamaha kwa kupitia taratibu za kisheria na wameitikia zaidi ya watu 467 na fedha Sh.  bilioni 107.842 zitaokolewa na nina uhakika hawatarudia makosa yao lakini nitoe tahadhari baada ya siku hizi saba kuisha wale wote watakaoshikwa kwenye makosa haya ya uhujumu uchumi sheria ichukue mkondo wake

“Nimetoa hizi siku saba na sitatoa nyingine lakini niwapongeze hawa 467 na mimi ningeomba ofisi ya DPP muharakishe ili watu waanze kutoka wakajumuike na familia zao kwasababu waliingia kwa njia ya mahaka watatoka kwa njia ya mahakama kwahiyo muwafikishe kwenye vyombo vya sheria ili waweze kuachiwa isije tena mtakapochambua mkakuta wamebaki 300,” amesema Magufuli.

Aidha amesema msamaha huo hautawahusu watuhumiwa wenye kesi mpya na kwamba wachukuliwe sheria kwakua msamaha huo ni kwa wale waliokwama tu.

“Watakaoshikwa na kesi za uhujumu uchumi leo, kesho na kuendelea wao waendelee na kesi zao za uhujumu uchumu maana huu msamaha hauwahusu hata kidogo kwani kuna wale ambao wana kesi mpya wao wapelekwe tu kwenye kesi,” amesema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com