Serikali ya Rwanda imekubali kuwapokea mamia ya wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi waliokwama nchini Libya.
Serikali ya Kigali imekubali kuwapokea wakimbizi hao wapatao 500 chini ya makubaliano ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.
Kwa mujibu wa Babar Beloch, msemaji wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, wakimbizi hao ambao aghalabu yao wanatokea katika nchi za Pembe ya Afrika wataanza kusafirishwa kwa ndege kuelekea Rwanda ndani ya wiki chache zijazo.
Amesema watahifadhiwa katika kituo kilichoko umbali wa kilomita 60 nje ya mji mkuu Kigali, na kwamba watakuwa huru kuingia na kutoka kwenye kituo hicho.
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limetahadharisha kuhusu hali mbaya ya wakimbizi nchini Libya.
Kwa mujibu wa UNHCR, kuna zaidi ya wakimbizi 4,700 wanaozuiliwa katika vituo mbalimbali nchini Libya, huku wengine 1,000 wakihifadhiwa katika kituo cha UN.
Social Plugin