Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Songwe
Serikali imepanga kubadilisha kilimo kutoka kuwa cha kujikimu na kuwa kilimo cha kibiashara kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 kwa kuzingatia mazao ya kipaumbele.
Miongoni mwa mazao hayo ya kipaumbele ni kahawa ambapo katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, Wizara ya Kilimo kupitia Bodi ya Kahawa imepanga kuongeza uzalishaji kutoka tani 65,000 hadi tani 80,000. Aidha bodi imepanga kuzalisha na kusambaza miche milioni 10 ya kahawa katika wilaya 42.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo tarehe 26 Septemba 2019 wakati akizungumza na watendaji wa Taasisi ya utafiti wa kahawa Tanzania (TaCRI) alipotembelea taasisi hiyo Mkoani Songwe.
Alisema kuwa zao hilo lina mchango mkubwa kwa uchumi wa Taifa na kwa maendeleo ya jamii lakini katika miaka ya karibuni lilionekana kuzorota kutokana na kuwapo kwa changamoto mbalimbali.
Kutokana na hali hiyo Serikali imeendelea kubuni mikakati mipya ya taratibu za usimamizi wa sekta hiyo ili kuleta ufanisi katika uzalishaji wa zao hilo.
Mhe Hasunga amesema kuwa ili kuongeza uzalishaji wenye tija katika zao la kahawa serikali imejipanga kuimarisha upatikanaji wa miche bora kwa ajili ya kuzisambaza kwa wakulima nchini.
Pia ameipongeza Taasisi hiyo kwa kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbegu bora za kahawa huku akisisitiza taasisi hiyo kuongeza weledi katika utoaji elimu kwa wakulima.
Naye, Mwenyekiti wa Taasisi ya utafiti wa kahawa Tanzania (TaCRI) Ndg Aloyce Mdalavuma ameiomba wizara ya Kilimo kwa ushrikiano na wataalamu mbalimbali wa TaCRI kuongeza juhudi ili kuongeza tija na uzalishaji wa kahawa.
Pia amesema kuwa uwezo wa Taasisi hiyo katika kuzalisha mbegu bora bado ni mdogo hivyo ameiomba serikali kuongeza uwezekano ili kuzalisha mbegu nyingi ambazo zitawafikia wakulima wengi.
Kwa upande wake Meneja wa kituo cha utafiti wa Kahawa Mkoani Songwe Ndg Isack Mushi ameeleza kuwa jukumu kuu la TaCRI ni kurudisha matumaini ya tasnia ya kahawa kwa kutoa na kusambaza teknolojia za kuendeleza zao la kahawa kwa ajili ya kuongeza tija katika uzalishaji na ubora.
Nyingine ni kupunguza gharama za uzalishaji, kuboresha kipato na riziki kwa wakulima wote wa kahawa na kuongeza mchango wa sekta ya kahawa kwenye pato la Taifa.
Social Plugin