Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUFUATILIA TOFAUTI YA MALIPO YA WALIOKUWA WAFANYAKAZI WA KIWANDA CHA MUTEX

Na. Peter Haule na Farida Ramadhani, WFM, Dodoma

Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina inaendelea na taratibu za kuwalipa waliokuwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Nguo cha Musoma (Musoma Textile Mills Limited Mutex) kwa mwaka wa fedha 2019/20, baada ya uhakiki kukamilika mwezi Juni, 2019.


Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Joyce Sokombi, aliyetaka kujua utofauti wa malipo kwa waliokuwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Mutex baada ya kufungwa mwaka 1984.

Dkt. Kijaji alisema kuwa, Serikali inafuatilia kwa karibu malalamiko yote yanayohusu tofauti ya kiwango cha malipo yaliyofanyika hivi karibuni ikilinganishwa na kiwango kilichoidhinishwa kwenye kikao cha pamoja kati ya Mfilisi wa Kiwanda hicho, wadau na Serikali ili kuona kama yana ukweli wowote.

“Baada ya Serikali kupokea maombi ya malipo kutoka kwa wafanyakazi hao mwaka 2018, Ofisi ya Msajili wa Hazina ilifanya uhakiki wa wafanyakazi hao ili kujiridhisha na hatimaye kufanya malipo”, alieleza Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa awali jumla ya wafanyakazi 219 walijitokeza na wasimamizi wa mirathi 14 na hivyo  kulipwa jumla ya Sh. milioni 44.5, pia Ofisi ya Msajili wa Hazina ilifanya tena zoezi la uhakiki mwezi Juni, 2019 kwa wafanyakazi ambao hawakujitokeza katika uhakiki wa awali  ambapo jumla ya wafanyakazi 115 walijitokeza pamoja na wasimamizi wa mirathi 22 ambao kwa ujumla wanastahili kulipwa takribani Sh. milioni 20.7.

Dkt. Kijaji alisema kuwa Serikali ilisimamisha uzalishaji katika kiwanda cha Nguo Mutex mwaka 1994 baada ya kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mtaji na ongezeko kubwa la madeni kutoka iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC)

Aliongeza kuwa Kiwanda cha Mutex kilifilisiwa na hatimaye kuuzwa mwezi Machi, 1998 kwa Kampuni ya LALAGO Cotton Ginnery and Oil Mills, kisha Wadai, Serikali na Mfilisi waliridhia mapendekezo ya kulipa kiasi cha Sh. milioni 161.3 kwa wafanyakazi 935 waliokuwepo kiwandani baada ya kikao kilichofanyika Septemba 23, 2005.

Alisema kuwa baada ya zoezi la ufilisi kukamilika, wafanyakazi 512 pekee ndio waliojitokeza kuchukua mafao yao na wafanyakazi 423 waligoma kupokea mafao yao kwa madai kwamba nauli ya familia na gharama za kusafirisha mizigo ni ndogo.

Wafanyakazi hao 423 walifungua kesi katika Mahakama ya Kazi ya Tanzania na baadae Mahakama hiyo ilitoa tuzo Juni 10, 2008 ambapo ilitupilia mbali shauri hilo na kuamuliwa wadai waende kwa mufilisi kuchukua stahili zao.

Aidha wadai hao walifungua shauri  jingine la maombi ya marejeo ambapo  Februari, 2010 Mahakama hiyo  iliamua tena wadai waliogoma kuchukua mafao yao waende kwa Mufilisi kama ilivyoridhiwa katika kikao cha wadau.

Mwisho


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com