Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SIMBA SC YAICHAPA MTIBWA SUGAR 2 -1 ...COASTAL NAYO YAIPIGA KMC 2-0 TANGA


Na Asha Said, DAR ES SALAAM
MABINGWA watetezi, Simba SC wameendeleza wimbi la ushindi baada ya kuichapa Mtibwa Sugar mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.

Pongezi kwa mshambuliaji aliyerejeshwa kikosini baada ya kuachwa kwa miaka kadhaa aende kupandisha kiwango chake kufuatia kuibuliwa timu ya vijana ya klabu, ‘Simba B’ Miraj Athumani ‘Madenge’ ama ‘Shevchenko’, au Sheva aliyefunga bao la ushindi akitokea benchi.

Na hiyo ni baada ya Simba SC kutangulia kwa bao la mshambuliaji kinara wa mabao, Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere aliyefunga bao la kwanza dakika ya 19 akimalizia krosi ya kiungo mpya, Msudan Sharaf Elidn Shiboub. 

Mtibwa Sugar wakasawazisha bao hilo dakika ya 21 kupitia kwa mshambuliaji wao chipukizi, Riphat Msuya aliyefunga kwa kichwa akimalizia mpira wa kona uliopigwa na kiungo Ismail Mhesa.

Na dakika saba tu baada ya kuchukua nafasi ya Hassan Dilunga uwanajani, Miraj akaifungia Simba SC bao la ushindi dakika ya 69 kwa shuti kali baada ya kupokea pasi ya Shiboub.

Mtibwa Sugar inayofundishwa na mchezaji wake wa zamani, Zubery Katwila ikapata pigo dakika ya 81 baada ya beki wake, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na kiungo Henry Joseph Shindika dakika nne baadaye.

Ushindi huo unaofuatia ushindi mwingine wa 3-1 dhidi ya JKT Tanzania kwenye mchezo wa kwanza, unaifanya SImba SC inayofundishwa na Mbelgiji Patrick Aussems ifikishe pointi sita na kupanda kileleni mwa Ligi Kuu, wakati Mtibwa wanapoteza mechi ya pili na zote ugenini, kufuatia kuchapwa 3-1 na Lipuli FC kwenye mchezo wa kwanza mjini Iringa.

Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Tairone Santos, Gerson Fraga, Clatous Chamadk/Francis Kahata dk79, Muzamil Yassin, Meddie Kagere, Sharaf Shiboub/Jonas Mkude dk90 na Hassan Dilunga/Miraj Athumani ‘Madenge’ dk62. 

Mtibwa Sugar; Shaaban Kado, Salum Kanoni, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’/Henry Joseph dk85, Cassian Ponera, Dickson Daudi, Abdulhalim Humoud ‘Gaucho’, Ally Makarani, Riphat Msuya, Ismail Mhesa/Abdul Haule dk81, Awadh Juma na Haruna Chanongo/Omar Hassan dk68.

Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, Coastal Union waliutumia vyema uwanja wa nyumbani, Mkwakwani mjini Tanga kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya KMC, mshambuliaji chipukizi Ayoub Lyanga akianza kumsetia Shaaban Idd kufunga la kwanza dakika ya 61 kabla ya yeye mwenyewe kufunga la pili dakika ya 72 akimalizia pasi ya Hassan Kibailo.
Via>>Binzubeiry

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com