Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SIMBACHAWENE AAGIZA WANAOHARIBU VYANZO VYA MAJI WACHUKULIWE HATUA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. George Simbachawene ameagiza wanaoharibu vyanzo vya maji katika maeneo yenye miinuko waondolewe mara moja na kuchukuliwa hatua kali za sheria.

 
Mhe. Simbachawene ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi wa Vijiji vya Chogola na Makosea wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani Mpwapwa katika Jimbo la Kibakwe ambapo alikemea tabia ya baadhi ya watu kukata miti kwenye maeneo yenye miinuko hali inayosababisha uharibu wa vyanzo vya maji.

Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo aliagiza watendaji wa kata na vijiji kuweka alama za mipaka kwa ajili ya kulinda vyanzo vya maji yenye umbali wa urefu wa mita 500 kila upande ili kuhakikisha wananchi hawavivamii.

"Tunapokata miti ya asili tunafanya maisha yetu kuwa magumu na vyanzo vya maji vinategemea uhifadhi wa misitu ya asili, inashangaza watu wanafyeka miti hadi kwenye milima kitakachotokea mvua ikinyesha kwa kasi ule udondo unaporomoka na kusababisha mmomonyoko wa udongo mtakuta kijiji chote kinasombwa," alitahadharisha.

Pamoja na hayo Simbachawene alibainisha kuwa changamoto ya mabadiliko ya tabianchi imesababisha mabadiliko ya misimu na hivyo kuleta athari kwa wanadamu kushindwa kuendesha shughuli za kilimo.

Aliongeza kuwa hali hii imechangia kubadilisha misimu na ndio maana wananchi wanalalamuka kukosa mvua za kutosha kuweza kufanya shughuli za kilimo.

Akiendelea kutoa elimu kwa wananchi Waziri Simbachawene alisema kitendo cha kukata miti kinaharibu ikolojia ya wanyama na mimea hali inayosababisha kukosekana kwa mvua na hivyo mabadiliko ya tabianchi.

"Tarehe 23 ya mwezi huu (Septemba), Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa marais wote kujadili namna nchi hizi zimezalisha hewa ya ukaa ambayo tunaita kaboni kutokana na shughuli zetu wenyewe.

"Hewa ya ukaa imeongezeka na kutengeneza joto gesi ambalo linatoboa anga la dunia ambayo ni 'ozoni layer' hali husababisha misimu kubadilika na hivyo ndo maana tunakabiliwa na changamoto ya mabadliko ya tabia nchi," alisema waziri huyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com