Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, ameongeza siku 7 zingine kwa watuhumiwa wa makosa ya Uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha, kuendelea kuwasilisha maombi ya kuomba radhi kwa Mkurugenzi wa mashtaka (DPP),ili waweze kusamehewa na kuachiwa huru.
Maamuzi hayo ameyatoa leo Septemba 30, 2019, Ikulu jijini Dar es salaam, wakati akipokea taarifa ya maombi ya Watuhumiwa wa Uhujumu Uchumi kutoka kwa DPP,ambapo hadi sasa jumla ya maombi 467 yamekwishawasilishwa.
"Najua una barua nyingine zimekwama kwenye Ofisi za Mkoa, na kama kweli wapo waliokwamishwa kwa sababu ya umbali, nimeongeza tena siku 7 ili usije ukaniomba tena, katika siku 7 wapo ambao walizuiliwa na Maofisa na Magereza akitaka hongo kidogo, Kamishina wa Magereza upo hapo mkafuatilie walioomba msamaha kwa DPP ili msiwakwamishe'' amesema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli ameongeza kuwa "natoa wito kwa Watanzania wenye tuhuma za uhujumu uchumi, wasiwe na wasiwasi ukishakiri basi kesho ndiyo ushahidi huo, siwezi nikafanya kazi ya kitoto ya namna hiyo nimeshasema nimetoa msamaha ni msamaha kweli, kwa hiyo wasidanganywe''
Mapema wiki iliyopita wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua, Rais Magufuli alishauri na kutoa siku 7 kwa DPP, kukutana na watuhumiwa wa uhujumu uchumi na kwa wale ambao watakuwa tayari kukiri makosa yao na kukubali kuzirudisha fedha hizo basi waachiwe huru.
TAZAMA HOTUBA YA RAIS MAGUFULI HAPA
Social Plugin