Mchungaji Gabriel Lugakingira
Na Lydia Lugakila -Malunde 1 blog
Waumini wa madhehebu mbalimbali,viongozi wa dini na viongozi wa serikali mkoani Kagera wametakiwa kujihadhari na matumizi ndimi zao ili kuepuka na kauli zinazoweza kusababisha migogoro isiyoisha katika jamii na nchi kwa ujumla.
Rai hiyo imetolewa leo Septemba 8, 2019 na Mchungaji Gabriel Lugakingira wa Kanisa la Kinjili la Kilutheri Tanzania KKKT mtaa wa Ibura wakati wa ibada ya Jumapili ilikwenda sanjari na maombi maalumu kwa ajili ya kuwaombea wanafunzi wanaotarajia kufanya mtihani kuhitimu darasa la saba mwaka 2019.
Mchungaji Lugakingira amesema muumini yeyote ama kiongozi yeyote anayetumia vibaya ulimi wake kwa kutoa kauli mbovu na kashfa ni chanzo kikubwa cha kuwepo kwa migogoro isiyoisha.
"Naomba tuchunge sana mdomo unaotoa kauli,mdomo unaweza kuunganisha watu na unaweza kufarakanisha ,tujihadhari na matumizi mabaya ya ndimi zetu",amesema.
Ameeleza kuwa ulimi huo huo umesababisha hata kudharauliana kiimani na hata kuchochea ubinafsi na jitihada za wanadamu zimeshindwa kuleta mafanikio katika dunia kutokana na kutumia ndimi vibaya huku akihimiza kutoka katika mitihani ya Ibilisi na kufuata mitihani ya Mwenyezi Mungu.