Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Picha : AGAPE YAIBUKA NA MRADI WA 'UTU WA MSICHANA'.. YAENDESHA MAFUNZO KUTOKOMEZA MIMBA NA NDOA ZA UTOTONI



Shirika lisilo la kiserikali la Agape Aids Control Programme la Mkoani Shinyanga, limeendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wazee wa dini, maarufu, pamoja na wa kimila wa kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, kwa ajili ya kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, pamoja na kutokomeza mimba na ndoa za utotoni ikiwa ni sehemu ya kutoa mchango katika mapango wa taifa wa kutomeza ukatili dhidi ya watoto na wanawake(MTAKUWWA).


Mafunzo hayo yameendeshwa leo Septemba 24, 2019 kwenye hoteli ya Liga Mjini Shinyanga,ikiwa ni sehemu ya utekelezaji mradi wa ‘UTU WA MSICHANA’ ambao unafadhiliwa na Shirika la Mundo Cooperante la nchini Hispania utakaotekelezwa ndani ya mwaka mmoja kwenye kata hiyo ya Mwamala.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Shirika hilo la Agape John Myola, amesema kitendo cha matukio ya ukatili kuendelea kuwepo ndani ya jamii imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo, ikiwamo kuzima ndoto za watoto wa kike, kwa kuwaozesha ndoa za utotoni na kukwamisha kufikia ndoto zao.

Amesema ili jamii ipate kuishi salama pamoja na kupata maendeleo, ni lazima waondokane na matukio ya ukatili pamoja na kuwekeza watoto wao kwenye elimu, ambao watakuja kupata kazi nzuri ama kujiajiri wenyewe, na kuweza kuwasaidia kuwa nyanyua kiuchumi kuliko kuzima ndoto zao kwa tamaa ya kupata mifugo.

“Jamii inapoendekeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ni kurudisha nyuma maendeleo, sababu utawanyima fursa ya kutekeleza majukumu yao ipasavyo , ikiwamo na watoto kushindwa kutimiza ndoto zao na kutokuwa tena tegemeo la taifa na familia kwa ujumla, na kubaki kuwa maskini,”amesema Myola.

“Familia ambayo haifanyi vitendo vya ukatili pamoja na kusomesha watoto wao huwezi kuikuta ina hali duni ya maisha, hivyo natoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga, kuwekeza watoto wao kwenye elimu ambapo watakuja kuwasaidia hapo baadae, na siyo kuwa ozesha ndoa za utotoni kwa tamaa ya mifugo,” ameongeza.

Naye Afisa mradi huo wa ‘UTU WA MSICHANA’ Sophia Rwazo kutoka Shirika la Agape, amesema  wameamua kuutekeleza mradi huo kwenye kata ya Mwamala, mara baada ya kufanya utafiti na kugundua kuwepo na tatizo la wanafunzi kupewa ujauzito pamoja na kulazimishwa kuozeshwa ndoa za utotoni.

Amesema mradi huo utakuwa ukitoa elimu ya madhara ya ukatili kwa wanawake na watoto kwa lika lote, wakiwamo wazazi, walimu, wanafunzi, wazee wa kimila, dini, Mabaraza ya watoto ya kata, Kamati za MTAKUWWA, pamoja na viongozi wote wa Serikali kwenye kata hiyo, lengo likiwa ni kuwapatia uelewa na kupinga kabisa vitendo hivyo, ili jamii iishi salama pamoja na wanafunzi kutimiza ndoto zao.

Aidha amesema mradi huo pia utawawezesha kupata elimu ya msingi na Sekondari kwa mfumo usio rasmi na kuwapeleka vyuo vya ufundi stadi wasichana ambao ni wahanga wa mimba na ndoa za utotoni pamoja na wale ambao wanaishi katika mazingira hatarishi ili kuweza kutimiza ndoto zao ambazo zilitaka kuzimwa sababu ya kufanyiwa vitendo vya ukatili.


TAZAMA PICHA HAPA CHINI

Mkurugenzi wa Shirika la Agape John Myola akizungumza kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wazee wa Kimila, Maarufu, Dini wakiwamo na viongozi wa Serikali kwenye kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga juu ya kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Picha zote na Marco Maduhu - Malunde 1 blog

Mkurugenzi wa Shirika la Agape John Myola akizungumza kwenye mafunzo hayo ambapo ameitaka jamii kuachana  na vitendo vya kukatisha ndoto za wanafunzi na kuwaozesha ndoa za utotoni.

Afisa mradi wa 'UTU WA MSICHANA kutoka Shirika la Agape Sophia Rwazo, akielezea namna mradi huo utakavyofanya kazi kwenye kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na hatimaye kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ikiwamo kutokomeza mimba na ndoa za utotoni.

Afisa mradi wa 'UTU WA MSICHANA Kutoka Shirika la Agape Sophia Rwazo, akiwataka wazazi kuacha tabia ya kubagua watoto wa kike kuwapatia elimu, bali wawasomeshe ili waje kuwasaidia hapo baadae.

Mwanasheria kutoka Shirika la Agape Suzy Mussa akielezea namna wazazi wanavyopaswa kutekeleza majukumu kwa watoto wao, kwa kuifuata sheria ya mtoto na kuachana na tabia ya kuwafanyia vitendo vya ukatili, ikiwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi.

Wazee wa kimila, wazee maarufu na viongozi wa kidini wakiwa kwenye mafunzo ya kuwajengea uelewa namna ya kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwenye kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Wazee wa Kimila, Maarufu na viongozi wa kidini wakiwa kwenye mafunzo ya kuwajengea uelewa namna ya kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwenye Kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Mafunzo yanaendelea

Mzee wa kimila Masanja Sunzula kutoka Kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga akichangia mada kwenye mafunzo.

Daudi Husein ambaye ni kiongozi wa dini kata ya Mwamala akichangia mada kwenye mafunzo.

Joseph Peter ambaye ni kiongozi wa Dini Kata ya Mwamala kutoka Kanisa la (EAGT) akichangia mada kwenye mafunzo.

Kazi ya vikundi ikiendelea kwa kupanga mpango kazi wa kwenda kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwenye Kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Kazi ya vikundi ikiendelea.

Kazi ya vikundi ikiendelea.

Kazi ya vikundi ikiendelea.

Mzee maarufu kata ya Mwamala Ngassa Maganga akiwasilisha kazi ya kikundi.

Mchungaji Joseph Peter kutoka kanisa la EAGT Mwamala akiwasilisha kazi ya kikundi.

Picha zote na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com