DC NDAGALA AONESHA DAWA YA KUKOMESHA MGOGORO KATI YA WAFUGAJI NA WAKULIMA KAKONKO


Na Rhoda Ezekiel - Malunde 1 blog
Wananchi wa vijiji vya Rusenga na Bukirilo wilayani Kakonko Mkoani Kigoma, wametakiwa kuacha tabia ya kuwakodishia mashamba wananchi wa nchi jirani ya Burundi kinyume na taratibu na wafugaji kuhifadhi ng'ombe wa raia wa nchi jirani hali inayopelekea kutokuwa na maelewano baina ya wafugaji na wakulima kwa sababu ya kugombania maeneo ingawa serikali ya vijiji hivyo imetenga maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji.

Rai hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Hosea Ndagala wakati akisikiliza kero za wananchi wa Vijiji hivyo ambapo walimlalamikia kuwepo kwa baadhi ya wafugaji wanaochukua ng'ombe kutoka Burundi na kuwaingiza katika maeneo ya kijiji na kudai ni wao na kulisha mashamba yao  huku wafugaji wakiwatuhumu wakulima kuwakata mapanga ng'ombe wao bila sababu.

Kanali Ndagala amekemea tabia hiyo ya viongozi wa vijiji pamoja na wananchi kukodisha mashamba maeneo ya mipakani kwa Warundi na pia wafugaji kuchukua ng'ombe wao na kuwahifadhi kijijini kinyume na sheria za nchi.

Kanali Ndagala aliahidi kuchukua hatua kali kwa yeyote atayebainika kufanya vitendo hivyo na pia atafanya oparesheni za kukamata ng'ombe wote wanaodaiwa siyo wa watanzania.

Alieleza kuwa migogoro ya wakulima na wafugaji katika vijiji hivyo inachochewa na viongozi wa kijiji, kwa kuwa viongozi hao wamejawa na rushwa hivyo aliwataka viongozi hao kuacha tabia hiyo na kuwasaidia wananchi kujua maeneo gani ni sahihi kwa ajili ya wakulima na maeneo gani ni ya wafugaji.

"Tumekuwa tukiwasisitiza wananchi mchague viongozi wasiopenda rushwa na waadilifu watakaowasaidia katika kutatua kero na kutatua migogoro lakini changamoto ninayoiona hapa chanzo kikubwa ni viongozi, msikubali kufanya makosa tunapokwenda katika uchaguzi ujao. 

Mkachague viongozi waadilifu wasiopenda rushwa, na kwa kuwa hapa tupo mpakani na mwingiliano ni mkubwa ni vyema kuwa makini katika kuchagua viongozi watakao simamia maagizo na maelekezo yanayotolewa," alisema Kanali Ndagala.


Aidha Kanali Ndagala aliwataka wakulima na wafugaji kuheshimiana kwamba mila mtu kuheshimu mali ya mwenzake, kwa kuwa wote wanategemeana na kuhakikisha hawaruhusu migogoro isiyo ya lazima kwa sababu kuna mwingiliano wa watu mpakani. 

Mmoja wa wafugaji Gidion Pascal alisema wao wamekuwa wakikamatiwa ng'ombe wao na wakulima muda mwingine wakulima wamekuwa wakikata mapanga ng'ombe na kupeleka kwenye serikali ya kijiji wao wanashindwa kuelewa wakulima wanalima kwenye maeneo yao na mifugo wao wakila mazao wanashitakiwa.

Alisema viongozi wa kijiji wakipatiwa na wakulima fedha wanawapatia kesi hivyo kuendelea kuweka uhasama kati ya wakulima na wafugaji kwa kuwa wakulima wanatumia nguvu ya ushawishi kwa kuwa ni wengi na viongozi wanapata fedha kutoka kwa wakulima kwa kuwakodishia mashamba ndiyo maana wanawanyanyasa.

Aidha aliiomba serikali kuhakikisha maeneo yaliyopangwa yanaendelea kuwa kama yalivyo wakulima wawe na maeneo yao na wafugaji wakae kwenye maeneo yao ilikuepuka migogoro na usumbufu baina ya wafugaji na wakulima na kuhakikisha viongozi wanasimamia hayo na kuacha kuchukua fedha za wananchi.

Naye Joseph Mgiligili alisema sababu kubwa ya kutokuwepo kwa maelewano ya wakulima na wafugaji ni viongozi kutokujua wajibu wao na mashamba hayo wanayolima ambayo yanadaiwa kuwa ni mali ya wafugaji waliuziwa na mwenyekiti wa kijiji hivyo wanaomba waonyeshwe sehemu sahihi ya kufanyia kilimo ilikuwaachia wafugaji eneo lao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Bukirilo Benson Ndenka alisema katika kijiji hicho yapo maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wakulima na wafugaji wapo baadhi ya wakulima ambao wanalima eneo ambalo sio sahihi na mazao yakiliwa wanalalamika.

Alisema watajitahidi kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri kwaajili ya wafugaji na wakulima kuhakikisha hakuna usumbufu na kuwazuia Wafugaji kuchukua mifugo nje ya nchi na kuileta kijijini hapo ambayo inasambaa na kula mazao ya wakulima na kupelekea ugomvi baina yao.
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akizungumza na wananchi wa Vijiji vya Rusenga na Bukirilo kata ya Gwanumpu wilayani Kakonko. Picha zote na Rhoda Ezekiel - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post