Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WALIMU 10 MBARONI TUHUMA ZA UDANGANYIFU MTIHANI WA DARASA LA SABA KAGERA...'WALIJIFUNGIA NDANI YA CHUMBA WAKI 'SOLVE' MASWALI YA SAYANSI'


Jeshi la  polisi Mkoani Kagera linawashikilia walimu 10 kwa tuhuma za kujihusisha na udanganyifu wa mtihani wa darasa la saba Wilayani Ngara Mkoani humo.


Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Septemba 13 mwaka huu kamanda wa polisi Mkoani Kagera Revocatus Malimi,alisema kuwa tukio hilo  lilitokea Septemba 12 Majira ya saa  4:40 katika shule ya msingi Kumnazi iliyopo tarafa ya Nyamiaga Wilayani Ngara.

Kamanda Malimi,alisema kamati ya mitihani ya wilaya  hiyo ilipata taarifa kuwa baadhi ya walimu watano waliokuwa wamejifungia ndani ya nyumba ya mmojawapo wa walimu hao waliokuwa na mtihani wa sayansi wakiandaa majibu kwa ajili ya kuwapa baadhi ya wanafunzi waliokuwa wakiendelea na mitihani ya taifa.

Aliwataja walimu wa shule ya msingi Kumnazi wanaoshikiliwa kuwa ni  Manase,Mtinange ( 50 ) mkuu wa shule hiyo,Prosper Pius ( 29 ),Joachimu Kakuru ( 31 ),Christiana Ilete ( 27 ) na Eric Balbati ( 30 ).

Alisema wasimamizi watano walioteuliwa kusimamia mitihani katika shule hiyo wanaoshikiliwa pia kwa mahojiano ni  Revocatus Juhudio ( 37 ) shule ya msingi Kashalazi, Jerusa Mganga ( 46 ) shule ya msingi Nyakahanga Rusumo,Rusalo Izaac maarufu Petro ( 31 ) shule ya msingi Kashalazi, Jofrey Mshahiri ( 31 ) shule ya msingi Mayenzi na Hezron Eugo ( 43 ) msimamizi mkuu wa kituo kizima .

Alisema idadi na majina ya watoto waliokuwa wanaandaliwa majibu ya mtihani na walimu hao imehifadhiwa kwa mujibu wa  sheria ya kulinda haki  za mtoto.

Alisema jeshi hilo  linaendelea na uchunguzi na uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtihani huo ulipatikana mazingira ya shuleni hapo.

Alisema kitendo kilichofanywa na watuhumiwa hao ni  kosa la  jinai kwa mujibu wa sheria.

Alisema mtihani ni  siri kuu  ya nchi licha ya kupewa semina na kula kiapo cha uadilifu ikithibitika wamehusika na udanganyifu wa aina yoyote wakifikishwa mahakamani adhabu yake  ni  kubwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com