Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WALIOFICHA MENO YA TEMBO WAPEWA MWEZI MMOJA WAJISALIMISHE

Na. Aron Msigwa – WMU, Dar es Salaam.

SERIKALI imetoa muda wa mwezi mmoja (kuanzia Septemba 4 hadi Oktoba 4, 2019) kwa wananchi wote wanaomiliki meno ya Tembo kinyume cha sheria, kuhakikisha wanayasalimisha kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na kwamba watakaofanya hivyo kabla ya kuisha kwa muda huo hawatashtakiwa.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ametoa muda huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es salaam mara baada Kikosi Kazi cha Taifa dhidi ya Ujangili (NTAP) kukamata watuhumiwa 8 wa ujangili, vipande 338 na meno mazima ya Tembo 75 pamoja  na meno mawili ya kiboko.

“Nimewaita hapa ili mshuhudie kazi nzuri iliyofaywa na maafisa wa Serikali na Kikosi Kazi maalum cha kudhibiti ujagili, ninatoa huruma ya mwezi mmoja kwa kila aliye na meno ya Tembo ayasalimishe kwenye chombo chochote cha Serikali na atakayefanya hivyo ndani ya muda huo hatutamshtaki” Amesisitiza Dkt.Kigwangalla.

Dkt. Kigwangalla amesema kukamatwa kwa majangili hao kumetokana na kazi ya muda mrefu ambayo imezaa matunda na matokeo yake kuonekana kwa kukamatwa kwa majangili sugu 8 (nane) akiwemo Bw. Hassan shaban maarufu kwa jina la Nyoni aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu kwa kujihusisha na mtandao wa ukusanyaji wa meno ya Tembo kutoka Tanzania na Msumbiji.

Amesema  mtuhumiwa huyo wa ujangili amekamatwa na jumla ya vipande vya meno ya Tembo 338 na memo mazima 75 pamoja pamoja na meno 2 ya Viboko ambapo kwa mujibu wa Wataalam na Wanasayansi wa Uhifadhi wa Wanyamapori wanaeleza kuwa meno hayo ni sawa na Tembo 117 waliouawa.

Amebainisha kuwa meno hayo yalianza kutafutiwa soko mwaka 2015 wakati Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ilipoingia madarakani, hivyo hatua ya Serikali kuimarisha  Ulinzi wa Rasilimali za Taifa  na kukiongezea uwezo Kikosi cha Kudhibiti Ujangili soko la meno hayo liliharibika.

Dkt. Kigwangalla amesema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya tano Majangili wengi wamekamatwa na mitandao yao kusambaratishwa akisisitiza kuwa yeyote atakayejihusisha na biashara hiyo kwa namna yoyote ile atakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria.

“Mtuhumiwa huyu amehangaika na huu mzigo kwa zaidi ya miaka minne na hili nataka watanzania wajue ya kwamba yeyote atakayejihusisha na biashara hii ya kuuza nyara za Serikali tutamkamata tu maana, sababu ni moja wateja tumebaki ni sisi wenyewe popote utakapojaribu kuuza tutakukamata tu”

Aidha, ametoa onyo kwa wananchi wanaojihusisha au kushiriki kwa namna yoyote ile  na vitendo vya ujangili waache mara moja akibainisha kuwa kazi hiyo kwa sasa haina nafasi nchini Tanzania.

Amesema kuwa kuanzia mwaka huu Wizara yake itaweka Mkakati mpya wa kukomesha vitendo vya ujangili nchini hadi kufikia mwaka 2014 akieleza kwamba mkakati huo utaimarisha kikosi kazi cha kudhibiti ujangili, kuimarisha ushirikiano na wizara nyingine, kuimarisha Jeshi USU na kuweka muundo mzuri utakaozuia mauaji ya wanyama.

Aidha, amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka 3 katika Ikolojia ya Selous hakuna Tembo hata mmoja aliyeuawa na majangili akibainisha kuwa meno ya Tembo yaliyokamatwa Agosti 31 mwaka huu ni yale ya ujangili uliofanyika nyuma kabla ya kuingia kwa Serikali ya awamu ya tano.

Amesema Kikosi Kazi hicho cha Serikali kimefanikiwa kuziba mianya yote ya biashara haramu za nyara za Serikali kwa kupambana na uharifu kwa kufuatilia na kusambaratisha mitandao yote ya ujangili ikiwemo mali na silaha za majangili.

Amebainisha kuwa kazi hiyo imefanikiwa kwa kuwa kinajumuisha maafisa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na vyombo vingine vya ulinzi na Usalama  na taasisi za kisheria  na kimekuwa kikifanya kazi nzuri ya kuratibu , kusimamia na kuchukua hatua za kupambana na uhalifu wa rasilimali za Wanyamapori na Mazao ya Misitu kwa kuendesha operesheni zinazoongozwa na taarifa za Kiintelijensia.

Dkt. Kigwangalla ameongeza kuwa Kikosi Kazi hicho kinafanya uchunguzi wa wahalifu na mali zinazotokana na uhalifu, kukamata, kupekua na kushikilia mali za wahalifu wanaojihusisha na ujangili.       

 “Sasa hivi kupitia Kikosi Kazi chetu tumeziba mianya yote, anayefanya biashara tutamkamata, aanayewinda kwenye maeneo ya hifadhi tutamkamata na hata askari wote wanaoshirikiana na majangili tutawakamata kwa kuwa tukimpata jangili mmoja tunahakikisha na mtandao wake wote tumeuvunja” Amesisitiza Dkt. Kigwangalla.

Dkt. Kigwangalla ameeleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2019 Kikosi Kazi hicho kimefanikiwa kukamata watuhumiwa zaidi ya 1072 silaha 539 zikiwemo siala 85 za Kivita na jumla ya risasi 37,921.

Aidha, nyara mbalimbali za Serikali zilikamatwa ikiwa ni pamoja na meno tembo, pembe za faru, ngozi za Simba, Chui na Duma, meno ya Kiboko, Kobe pamoja na mazao ya Misitu.

Pia Dkt. Kigwangalla amebainisha kuwa Kikosi kazi hicho hadi sasa kimefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wakubwa wa ujangili wakiwemo Aloyce Francis Ayubu( Kamanda),  Mateso Kassiani Albano (Mateso Chupi)  na Jayzan George Kuchar (China), Haruna Kassa, Frank Silagei na Ojugu (Original).

Wengine ni Haong Nghia Trung, MS. Yang Feng Glan (Queen of Ivory) ambaye amekwishahukumiwa pamoja na Salvius Francis Matembo na Manase Julius Philemon, Boniface Maringo, (shetani), Juma Maringo (Yesu), Godfrey James Nyamicha (Papa), Haidari Omary Sharif, Oliva Lucas Mchua na Mrangilwa Emanueli.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com