Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI HASUNGA APIGA MARUFUKU KUFUNGA MIPAKA YA UUZAJI MAZAO

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema kuwa serikali haikusudii kufunga mipaka ya uuzaji wa mazao hivyo wafanyabiashara wana ruksa ya kuuza mazao popote watakapo.



Mhe Hasunga ameyasema  tarehe 13 Septemba 2019 wakati akizungumza na wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo katika katika ofisi ndogo Jijini Dodoma.

Waziri Hasunga amesema kuwa wizara hiyo haitapiga marufuku usafirishaji na uuzaji wa mazao ya kilimo nje ya nchi na haina mpango wa kuweka katazo hilo ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa soko la wakulima kwa kuwa Taifa lina chakula cha kutosha.

Mhe Hasunga, ametoa wito kwa wakulima na wafanya biashara wanaojishughulisha na kununua au kuuza mazao ya kilimo kuendelea na biashara yao  ili kuongeza tija kwa wakulima.

Aidha, amewataka wakulima kuendelea kuchangamkia fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi ambazo zina upungufu au uhitaji wa mazao hayo.

Alisema kuwa jukumu kubwa la serikali ni kuhakikisha kwamba taifa linajitosheleza kwa chakula na kilimo kinaendelea kutoa ajira kwa watanzania walio wengi.

“Wakati mkulima anahangaika na kilimo mlishirikiana nae, wakati anahangaika kulima mlimpelekea pembejeo, wakati anavuna mlishirikiana nae, lakini sahizi mnataka kuleta masharti ya nini” Alihoji Mhe Hasunga

Awali akizungumza kwenye mkutano huo Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba amesema kuwa ili kilimo kiwe na tija ni lazima serikali ijikite katika miundombinu ya barabara hasa vijijini ili mazao ya wakulima yaweze kufika sokoni kwa wakati hiyo ndiyo sababu ya bajeti ya serikali kujikita katika kujenga miundombinu ya barabara.

Hata hivyo amewataka wafanyakazi wa serikali na wizara ya kilimo kufanya kazi zenye viwango bila kuangalia kiwango cha mshahara wanaolipwa kwani baada ya serikali kuyafanya maendeleo mishahara itapandishwa.

Aidha, ameongeza kuwa vijana waliopelekwa Israeli kwa ajili ya mafunzo itakuwa vyema kama watapelekwa kwenye Halmashauri au kwa wakulima kwa ajili ya kwenda kuonyesha kwa vitendo teknolojia walizo jifunza kwa kuwasaidia  wakulima kuboresha kilimo chao.

Naya Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Hussein Bashe amewataka watendaji hao kuongeza tija na uzalishaji katika kilimo kwani kwa sasa serikali imejipanga katika kukuza sekta ya viwanda hivyo ni lazima mazao ya kilimo yatakayo hitajika yawe yana ubora na yakutosha.

Alisema kuwa watendaji hao hawapaswi kuangalia upungufu wa vifaa na miundombinu ya kufanyia kazi badala yake wanapaswa kuongeza juhudi kuhakikisha kuwa wanaandaa vitu vyenye ubora.

“Waziri hawezi kwenda kwa Dokta Mpango kuomba hela kwa ajili ya kuwekeza kwenye eneo fulani hata pata kama ubora wa kile kitu hauonekani” Alisisitiza Mhe Bashe

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com