WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ifuatilie kwa karibu miradi nane iliyowasilishwa na kuombewa fedha za ufadhili kupitia mkutano wa saba wa TICAD uliofanyika Agosti 28-30, 2019 jijini Yokohama, Japan.
“Kupitia Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo Kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7), Serikali ya Japan imetenga kiasi cha dola za Marekani bilioni 20 kwa kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya nchi za Afrika. Ninaielekeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ishirikiane kwa karibu na Wizara zenye dhamana kuratibu vema utekelezaji wa miradi nane ya maendeleo ambayo tayari imewasilishwa kupitia TICAD 7,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Septemba 13, 2019) katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa kuahirisha Mkutano wa 16 wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Novemba 5, mwaka huu.
Amesema fedha hizo zimetengwa ili kuziwezesha nchi za Afrika zitekeleze miradi ya kimkakati ya maendeleo itakayoleta mageuzi ya kiuchumi. “Kiasi hicho kitatolewa ili kuendeleza miradi mbalimbali katika sekta za elimu, afya, kilimo, maji, nishati, ujenzi wa maeneo maalumu ya viwanda na miundombinu ya usafiri na usafirishaji.”
Amesema lengo la Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha Tanzania inanufaika na fedha hizo zilizotengwa na Serikali ya Japan ili iweze kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka Watanzania watumie fursa ya upungufu wa nafaka katika nchi za Kusini mwa Afrika kwa kuzalisha zaidi mazao hayo ikiwa ni pamoja na kujiwekea akiba zaidi.
Amesema hali ya usalama wa chakula katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), imetetereka kutokana na athari mbalimbali ikiwemo ukame katika upande wa magharibi wa ukanda, mvua zilizokithiri, mafuriko na vimbunga vya IDAI na Kenneth pamoja na wadudu waharibifu wa mazao na magonjwa.
“Athari hizo zimesababisha uzalishaji wa nafaka kama mahindi, mtama, mpunga, ngano na ulezi ndani ya SADC upungue kwa asilimia 14 kutoka tani milioni 42.6 mwaka 2018 hadi tani milioni 36.8 mwaka 2019. Hata hivyo, Tanzania na Afrika Kusini kwa kipindi hicho zilizalisha ziada ya mazao hayo ambayo yanakadiriwa kukidhi mahitaji kwa mwaka 2019/2020,” amesema.
Waziri Mkuu amesema kuwa Agosti 29-30, mwaka huu, Wizara ya Kilimo iliratibu mkutano na wadau mbalimbali wenye kujihusisha na uzalishaji na biashara ya nafaka ili kujadili fursa zilizopo katika mazao ya nafaka, changamoto wanazokabiliana nazo na kutafuta utatuzi wake.
“Ninaigiza Wizara husika ihakikishe inashirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili kutumia vema fursa ya uwepo wa masoko ya nafaka kwenye ukanda huu wa SADC na hivyo, kukidhi mahitaji katika ukanda sambamba na kuboresha biashara na maisha ya wananchi wa vijijini,” amesema.
Pia ameitaka wizara hiyo iendelee kuhamasisha uzalishaji wa mazao hayo kwa wingi ili nchi iweze kujitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Social Plugin