WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi na Halmashauri ya Mji wa Mafinga wahakikishe wanajenga mradi wa kimkakati kwa kutumia fedha za mapato ya ndani na si kusubiri miradi kutoka Serikali Kuu wakati wanakusanya zaidi ya sh. bilioni saba kwa mwaka.
Amesema halmashauri hizo licha ya kukusanya fedha nyingi kwa mwaka lakini matumizi yake si mazuri kwa sababu hawana mradi wowote wa kimkakati wanaoutekeleza, mfano ujenzi wa maeneo ya kuegeshea magari makubwa au hata ujenzi wa kituo cha mabasi, miradi ambayo ingewaongezea mapato.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Septemba 26, 2019) wakati akihutubia na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Wambi wilayani Mufindi akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Iringa.”Nataka kuona mradi wa kimkakati ukitekelezwa kwa fedha mnazokusanya kutoka kwa wananchi.”
Alisema viongozi hao wanaweza kutenga kiasi cha sh. bilioni moja kwa mwaka na kujenga hospitali au wakatenga fedha na kujenga barabara za lami kwa awamu katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga kwa kuwa ujenzi wa barabara za lami mijini ni sh. milioni 300 kwa kilomita moja, hivyo wangeweza kutekeleza ujenzi huyo kutokana na fedha wanazokusanya.
“Msitegemee fedha kutoka Serikali Kuu tu jengeni wenyewe barabara zenu kuzunguka Mji wa Mafinga kwa kiwango cha lami kwa sababu mna fedha za kutosha tena mnaweza kutumia fedha za mapato ya ndani mnazokusanya kutoka kwa wananchi badala ya kuzitumia kwa kulipana posho tu.”
Awali,Waziri Mkuu alitembelea shule ya Sekondari ya kata ya Mdabulo na kupokea taarifa fupi ya ujenzi wa bwalo, bweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike pamoja na ujenzi wa madarasa na kisha alizungumza na wananchi na kuwaeleza miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kwenye maeneo yao.
Waziri Mkuu alisema katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya karibu na maeneo yao ya makazi, Serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa vituo vya afya katika kila kata pamoja na ujenzi wa hospitali za wilaya ikiwemo na wilaya yao ya Mufindi ambayo ipo katika hatua mwisho kukamilika.
Kwa upande wao, wabunge wa mkoa wa Iringa wakiwemo wa majimbo na wa viti Maalumu kwa nyakati tofauti waliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kutoa fedha za ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye mkoa wao.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Social Plugin