Na. Josephine Majura na Farida Ramadhani
Serikali imeitaka Benki Kuu ya Tanzania- BOT kufanya utafiti wa Taasisi za kifedha hasa taasisi ndogo nchini kuona kama kweli riba wanazotoa kwa wateja wao zina sababu ya msingi au zinatolewa kwa riba kubwa kwa kujilimbikizia faida kubwa na kuwaumiza wateja, wakiwemo wajasiriamali na watumishi hasa wa kada ya chini.
Rai hiyo imetolewa Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, wakati akifungua hafla ya kugawa Hati za viwanja kwa wanachama wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo- Hazina Saccos.
Dkt. Mpango amezitaka Benki na taasisi ndogo za fedha nchini kuangalia upya namna ya ukokotoaji wa riba kwa kuwa zinawaumiza wananchi wakiwemo wajasiriamali na watumishi ambao wanazitegemea katika kupata mitaji yao.
“Kuna Taasisi moja ambayo inakopesha fedha kwa watumishi wa Serikali akiwemo Walimu, kwa riba ya asilimia 32 ilihali wao wanachukua mikopo Benki kwa asilimia 20 ni hatari kweli, asilimia 32 ni riba kubwa mno”, alisisitiza Dkt. Mpango
Alisema kuwa mchango wa SACCOS unatambulika kama nyenzo muhimu ya kupunguza umasikini, ndio maana Serikali imetunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha kwa ajili ya kuzisimamia taasisi ndogo za fedha ili kuwapunguzia adha wafanyakazi na wajasiriamali wanaokopa fedha katika taasisi hizo kwa riba kubwa na masharti ya kinyonyaji.
Dkt. Mpango aliwasihi viongozi wa SACCOS zote nchini kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, weledi na kutumia maarifa ili kufanikisha ndoto za wanachama wao kwa kuwa SACCOS ndio kimbilio kwa watumishi wengi hasa wa kada za chini.
Alisema kuwa kunachangamoto ya ubadhilifu katika SACCOS nyingi nchini, jambo ambalo asingependa kulisikia kwa Hazina Saccos ambayo yeye pia ni mwanachama, hivyo ameitaka Saccos hiyo pamoja na nyingine kujitahidi kuweka mifumo imara ambayo itawezesha kutambua upotevu wa mali za Saccos ili kuweza kudhibiti mapema kabla ya madhara makubwa kujitokeza.
Waziri huyo amewataka wanachama wa Hazina Saccos kuchangamkia fursa za kiuchumi na zingine zilizopo katika Jiji la Dodoma kwa manufaa binafsi na taifa kwa ujumla.
Aidha ameitaka Saccos hiyo kuendelea kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wanachama na atafurahi iwapo Hazina Saccos itakuwa mfano kwa Saccos nyingine katika uadilifu na kujali masilahi mapana ya wanachama wake ili kuchochea shughuli za maendeleo zenye tija kwa taifa.
Amewataka Wanachama wa vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo kuacha tabia ya kutorudisha mikopo kwa wakati kwa kuwa inarudisha nyuma maendeleo ya Saccos.
Naye Mwenyekiti wa Bodi wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina (Hazina SACCOS), Bw. Aliko Mwaiteleke, alimuomba Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) aweze kukisaidia chama hicho kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili ikiwemo suala la mipaka ya eneo walilonunua ambako miundombinu ya reli ya kati imepita.
Alisema katika eneo walilonunua kuna sehemu ambayo imeingia katika mradi wa reli ya kati lakini bado hawajaoneshwa mpaka wa wapi mradi huo unaishia ili kuwawezesha wamiliki wa eneo hilo kuanza kuliendeleza.
Pia Bw. Mwaiteleke alimuomba Dkt. Mpango, akiunganishe chama hicho na vyanzo vya fedha ili kiweze kupata mikopo nafuu kwa maendeleo ya chama na wanachama kwa ujumla.
Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina (Hazina SACCOS) kilianzishwa mwaka 1972 kikiwa na wanachama 100 na kusajiliwa kisheria mwaka 1973. Kwa sasa kina wanachama 5600 na kinaongozwa na Sheria ya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013.
Social Plugin