Na Mathias Canal, Jerusalem-Israel
Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Japhet Hasunga (Mb) leo tarehe 5 Septemba 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Wakurugenzi 6 wa Mashav wa Wizara ya Mambo ya nje ya Israel.
Katika mkutano huo wa kazi uliofanyika katika Ofisi za wizara ya Mambo ya nje ya Israel iliyopo mtaa namba 9 Yitzhak Rabin Jijini Jerusalem nchini Israel, Waziri wa Kilimo amewasilisha mambo mbalimbali kuhusu sekta ya kilimo ikiwemo ufuatiliaji wa utekelezaji wake.
Mhe Hasunga ameishukuru serikali ya Israel kwa kukubali ombi la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli la kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoshiriki mafunzo ya Kilimo ya Agro Studies katika kipindi cha mwaka mmoja kutoka 45 ambapo imefikia idadi ya wanafunzi 100.
Katika kikao hicho Waziri Hasunga amewakumbusha Mabalozi hao sita kuhusu ombi la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli la kuongezwa idadi ya wananfunzi kufikia idadi ya wanafunzi 300.
Mhe Hasunga amesema kuwa Balozi huyo amepongeza kwa dhati na kuunga mkono juhudi za serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe Dkt John Pombe Magufuli kwani ni serikali ya vitendo na uwajibikaji hivyo wapo tayari kuhakikisha kuwa ushirikiano unaboreshwa baina ya nchi hizo mbili.
Kikao hicho pia kimejadili kwa kina namna ya kuboresha zaidi mahusiano baina ya nchi ya Tanzania na Israel hususani katika kuimarisha ushirikiano kwenye nyanja za utafiti, uongezaji thamani wa mazao, na namna ya kuongeza ukubwa wa mashamba na kilimo tija.
Pia, Mhe Hasunga amewasilisha ombi la kupata kampuni mbalimbali za nchini Israel ili kuzuru Tanzania na kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji.
“Tukipata kampuni za kuisaidia Tanzania kwenye maswala ya kilimo cha umwagiliaji tutakuwa na fursa ya kubadili kilimo chetu kutoka kwenye kilimo cha kutegemea mvua na hatimaye kuingia katika kilimo cha umwagiliaji” Alisisitiza Mhe Hasunga na kuongeza kuwa
Serikali ya Israel imekubali kufikiria kuongeza idadi ya vijana kutoka Tanzania wanaozuru Israel kwa ajili ya kujifunza ambapo pia wataongeza uwezekano wa wataalamu mbalimbali wakiwemo maafisa ugani nchini Tanzania kuzuru Israel kwa ajili ya kujengewa uwezo katika utendaji.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Maendeleo ya Ushirikiano wa mambo ya nje nchini Israel Ndg Yuval Fuchs amesema kuwa serikali ya Israel imeridhia maombi ya Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Japhet Hasunga na kusema kuwa Israel ipo tayari kushirikiana na Tanzania ili kuboresha sekta ya kilimo kutoka kwenye kilimo cha kujikimu kuwa kilimo cha kibiashara
Vilevile amesema kuwa atazishawishi kampuni mbalimbali kuwekeza nchini Tanzania kwa ushirikiano mzuri na serikali kwani Tanzania kuna ardhi nzuri yenye rutuba kwa ajili ya kilimo.
Kadhalika amempongeza Waziri Hasunga kwa kutembelea nchini Israel kwa ajili ya ziara ya kikazi ambapo amesema kuwa kumekuwa na kikao muhimu kilichojadili namna ya kuboresha kilimo nchini Tanzania.
Kadhalika, Balozi wa Tanzania nchini Israel Balozi Job Daud Masima amesema kuwa kikao cha Waziri wa Kilimo ni muendelezo wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo nchini Israel ambapo ameongeza kuwa kikao hicho kimetoa taswira ya kutafakari kwa pamoja kuona namna mafunzo hayo yanavyowasaidia vijana wa kitanzania.
Amesema Waziri Hasunga amekutana na ujumbe wa mabalozi 6 pamoja na wasaidizi wake wanaohusika na maswala ya Afrika Mashariki, kikao hicho kimetoa heshima kubwa kwa serikali ya Tanzania ambapo vijana 100 watapokelewa nchini Israel na waziri Hasunga leo tarehe 5 Septemba 2019.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya agrostudies Ndg Yaron Tamir amesema kuwa wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo kutoka Tanzania wametoa ushirikiano mzuri hivyo mafunzo hayo waliyoyapata wanapaswa kuyaendeleza ili kuboresha kilimo nchini Tanzania.
MWISHO
Social Plugin