Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS MUSEVENI : MBUNGE BOBI WINE NI ADUI WA UGANDA

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amemtaja mkosoaji wake mwanamuziki aliyegeuka kuwa mwanasiasa Bobi Wine, kama "adui wa mafanikio ya nchi".

Rais Museveni ameyasema hayo katika mahojiano na BBC.

Bwana Museveni anataka kugombea muhula wa sita kama rais mnamo mwaka 2021 baada ya kuwa rais wa nchi hiyo kwa miaka 33.

Bobi Wine, ambaye ni kiongozi wa vuguvugu la 'The People Power', anamshutumu rais huyo kwa kuongoza kwa mfumo wa ukandamizaji.

Bwana Museveni amekataa kumueleza mwandishi wa BBC , Alan Kasujja ikiwa serikali yake ni ya ukandamizaji , lakini akasema anamshughulikia Bobi Wine kama adui.Rais wa Uganda amesema ataendelea kuwa madarakani zaidi ili kushughulikia matatizo ya Uganda na Afrika

Rais huyo wa Uganda amemlaumu Bobi akisema kuwa alikwenda Marekani na kusema kwamba watu wasije kuwekeza Uganda: ''Unapoenda na kuwaambia wageni kwamba hawapaswi kuja na kuwekeza katika nchi yetu, inamaanisha umeanzisha vita dhidi ya mafanikio yetu. Kwa hiyo kwa nini sasa unataka kurejea na kunufaika na mafanikio hayo?".

Hii huenda ndio moja ya sababu za kufutwa kwa matamasha ya muziki ya Bobi Wine, bado sijaongea na polisi kupata taarifa zaidi, alisema.

Juhudi za Bobi Wine kuhamasisha umma dhidi ya rais Yoweri Museveni zimekuwa zikizimwa na maafisa wa usalama

Rais huyo wa Uganda anasema bado ataendelea kuwepo madarakani kwa miaka mingine zaidi kukamilisha kile ambacho yeye binafsi na wapiganaji wenzake walikipanga kukifanikisha katika nchi yao na Afrika.

''Nyumba yangu inanisubiri, lakini tuna masuala kama Uganda ya kushughulikia. Ni masuala hayo ambayo yanatufanya tufanye kile tunachotaka kukifanya kisiasa pamoja na wenzetu. Kama chama tawala (NRM) kitafikiria kuwa hakihitaji mchango wa wazee basi tutaondoka madarakani kwa furaha na kufanya mambo mengine ." Museveni alimueleza mwandishi wa BBC Allan Kasujja mjini Kampala.

''Hatupo hapa kwa ajili ya maonyesho, hatuendi kwenye ukumbi wa michezo ya maigizo , sisi ni watu ambao tupo hapa kushughulikia masuala makubwa ya Uganda na Afrika ." Alisistiza kiongozi huyo wa Uganda.

Kiongozi wa upinzani Dkt Kizza Besigye alikabiliwa na nguvu ya maafisa wa usalama kila alipojaribu kuonyesha upinzani dhidi ya serikali ya Museveni

Rais Yoweri Museveni ambaye amekuwa madarakani Uganda sasa kwa zaidi ya miongo mitatu.

Bwana Museveni amekuwa akikabiliwa na miito ya kumtaka ajiuzulu hasa kutoka kwa vijana na wapinzani wake .

Mpinzani wake wa muda mrefu Dkt Kizza Besigye amepitia misukosuko mingi katika harakati zake za kisiasa pamoja na Mbunge Bobi Wine ambaye juhudi zake za kutumia usanii wake wa kimuziki kuhimiza ajiuzulu zimekuwa zikizimwa na maafisa wa usalama.

Chanzo - BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com