AFDB KUIPATIA TANZANIA ZAIDI YA SHILINGI TRILIONI 1.5 KUJENGA UWANJA WA NDEGE MSALATO

Na Mwandishi wetu, Abidjan, Ivory Coast.

Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imepongeza uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wa kuhamia Dodoma na kuahidi kuidhinisha kiasi cha dola za kimarekani milioni 455 sawa na zaidi ya shilingi za Kitanzania trilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato sambamba na ujenzi wa barabara za mzunguko Jijini  humo.

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina ameyasema hayo katika Ofisi za Makao Makuu ya Benki hiyo yaliyopo Abijdan Nchini Ivory Coast wakati wa Mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi na kuongeza kuwa benki hiyo itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Rais Dkt John Pombe Magufuli katika kipindi chake cha Uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) lakini pia kwa Tanzania.

Amesema Benki hiyo tayari imeshaidhinisha kiasi cha dola za marekani milioni 180 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mzunguko jijini  Dodoma na kwamba kiasi kingine cha dola za marekani milioni 275 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato kinatarajiwa kuidhinishwa na mapema mwezi Novemba 2019.

Dkt. Adesina ameongeza kuwa Benki ya Maendeleo ya Afrika ina imani na mageuzi ya kiuchumi yanayotekelezwa chini ya Uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo elimu bila malipo,afya na maji pamoja na mapambano dhidi ya rushwa na kuleta uwajibikaji katika taaisisi za uma na kwamba iko tayari kuunga jitihada hizo za serikali kwa kuwekeza katika sekta ya miundombinu.

Aidha Dkt. Adesina ameelezea nia yake ya kutaka kushudia bara la Afrika likipiga hatua kubwa za kimaendeleo sasa na kwa haraka na sio kusubiri baadae na kwamba katika kipindi chake cha uongozi katika Benki ya Maendeleo ya Afrika atapambana kuhakikisha azma hiyo inatekelezeka.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ushirikiano inayoutoa kwa Tanzania hususani katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambayo kimsingi yalikuwa ni maono ya Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere kwa nia ya kuiwezesha Tanzania kujitegemea kiuchumi na hatimae Bara zima la Afrika.

Prof. Kabudi ameongeza kuwa tayari Benki ya Maendeleo ya Afrika iko tayari kufadhili ujenzi wa reli ya kisasa yaani Standard Gauge Railway ya kipande cha kutoka Isaka hadi Kigali nchini Rwanda na kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mara baada ya kukamilika mchakato wa utoaji wa fedha hizo ambapo mazungumzo ya awali kuhusu ufadhili huo yameanza.

Pia Prof. Kabudi amemtaka Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Dkt. Akinwumi Adesina kuimarisha ofisi za kanda za benki hiyo ili ziweze kutoa huduma zote za kibenki ili kusogeza huduma karibu na wanufaika wa benki hiyo sambamba na kuunga mkono miradi yote ya kimkakati inayounganisha nchi na nchi katika bara la Afrika ili kuboresha nakurahisisha huduma ya usafiri katika Bara la Afrika na hivyo kuwezesha biashara miongoni mwa nchi za Kiafrika na kujiletea maendeleo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi yuko Abijdan Nchini Ivory Coast kushiriki mkutano wa siku mbili wa dharura wa Mawaziri wa fedha uliondaliwa na Benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB).


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post