Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha akizungumza na watumishi wa idara ya afya ya halmashauri ya Ushetu waliohudhuria Mafunzo hayo.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo ambao ni watumishi wa idara ya afya wa Halmashauri ya Ushetu wakimsikiliza kwa Makini mkuu wa wilaya ya Kahama.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo ambao ni watumishi wa idara ya afya wa Halmashauri ya Ushetu wakimsikiliza kwa Makini mkuu wa wilaya ya Kahama.
**
Na Salvatory Ntandu - Malunde 1 blog
Serikali wilayani Kahama mkoani Shinyanga imesema itachukua hatua kali kwa watumishi wa sekta ya afya katika halmashauri ya Ushetu watakaobainika kuhujumu Mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za utaoaji wa huduma za afya (GOT-HOMIS) kwa njia ya kielekroniki ambao umezinduliwa rasmi katika Halmashauri hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha katika hafla ya kufunga mafunzo ya siku tatu kwa watumishi wa sekta ya afya ambayo yametolewa na maafisa Tehama kutoka mkoa wa shinyanga ambayo yamelenga kuboresha sekata ya afya na kupunguza malalamiko kutoka kwa wagonjwa.
Amesema serikali ya awamu ya tano imelenga kuondoa kero kwa wananchi na endapo Mfumo huo ukisimamiwa vizuri utaweza kupunguza malalamiko kutoka kwa wagonjwa pindi wanapokwenda kupatiwa huduma za afya katika Zahanati na vituo vya afya sambamba na utunzaji sahihi wa taarifa ambazo zitasaidia kupata takwimu za utendaji kazi wao.
“Mfumo huo unasaidia kutunza kumbukumbu za upatiakanaji wa dawa na pamoja na udhibiti wa fedha ambao hapo awali watumishi wa sekta ya afya walikuwa wanatumia vitabu kwaajili ya kutolea stakabadhi na badala yake kwa sasa watalazimika kutumia mashine maalumu”,amesema Macha.
Nae Mganga mkuu wa Halmashauri ya Ushetu Dk Nikodemas Senguo amesema kukosekana kwa huduma ya nishati katika maeneo mengi katika zahanati na Vituo vya afya huenda ukaisha utendaji kazi wa mfumo huo kutokana na maeneo mengi kutumia mfumo wa umeme wa jua.
Amesema kuanzia sasa kila zahanati na kituo cha afya vitakuwa vinatumia mfumo huo na kuondokana na matumizi ya vitabu kwaajili ya kuingiza taarifa za wagonjwa ambao unaenda sambamba na ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa njia ya kielektroniki.
Jumla ya zahanati 22 na vituo vitatu vya afya vimeshagawiwa kompyuta kwaajili kuanza kutekeleza mfumo huo wa kielekroniki katika halmashauri ya Ushetu.