Na Walter Mguluchuma - Malunde 1 blog Katavi
Watu wanne wakazi wa tarafa ya Mamba Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi wamehukumiwa kwenda jela kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kutaka kumuua mtu mwenye ualbino kwa kumkata mkono wake na kisha kuondoka nao kwa lengo la kwenda kuuza kwa mganga wa kienyeji.
Waliohukumiwa kifungo hicho cha maisha kuanzia jana ni Alex Manyanza Nogele Maliganya , Galila Nkuba (Malago) na Shile Dalushi wote wakazi wa tarafa ya Mamba Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi
Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Richard Wilbrod Mashauri wa Mahakama kuu ya Kanda ya Sumbawanga katika Mahakama ya Hakimu mkazi ya Mkoa wa Katavi baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani ambapo upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi kumi na mbili.
Katika kesi hiyo ilisikilizwa na Mahakama kuu ya Kanda ya Sumbwanga upande wa mashitaka uliwakilishwa na wanasheria wa serikali wawili Simon Peres na Dickson Elias Makoro na washitakiwa walitetewa na mawakili wawili Elias Kifunda na Patrick Mwakyusa.
Awali katika kesi hiyo waendesha mashitaka wanasheria hao wa serikali walidai kuwa washitakiwa hao wote kwa pamoja walidaiwa kutenda kosa hilo Mei 14 mwaka 2015 katika kijiji cha King'anda tarafa ya Mamba majira ya saa sita usiku.
Imelezwa kuwa siku ya tukio watuhumiwa hao walikwenda nyumbani kwao na mtu mwenye ualbino aitwaye Lime Luchoma ambaye alikuwa amelala chumbani ndipo washitakiwa hao walipojaribu kumuua kwa kumkata mkono wake wa kulia na kisha kuondoka na mkono huo kwa lengo la kwenda kuuza kwa mganga wa kienyeji kwa gharama ya shilingi milioni sita.
Walidai kuwa baada ya kuwa wamechukua mkono wa Lime Luchoma waliondoka nao na kisha walikwenda kuubanika kwenye moto ili iwe rahisi kwao kwa kuweza kuusafirisha na kwenda kuuza kwa mganga wa kienyeji aliyekuwa amewaagiza wamtafutie.
Katika utetezi wao Mahakamani hapo washitakiwa hao waliiomba Mahakama iwaachie huru kwani maelezo yao waliyoyatoa mbele ya mlinzi wa amani katika Mahakama ya Mwanzo ya Mpanda Mjini ambayo walikiri kufanya kitendo hicho walidai walikubali kosa hilo kwa kuwa walikuwa wamepata mateso ya kupigwa na polisi.
Washtakiwa wote wanne wamepatika na hatia ya kifungu cha sheria 211(a) cha sheria ya adhabu sura namba 16 marekebisho ya mwaka 2002.
Jaji Mashauri alieleza kutokana na washitakiwa kupatikana na kosa hilo Mahakama kuu imewahukumu washitakiwa hao wanne kutumikia jela kifungo cha maisha na kama hawajaridhika na hukumu hiyo wanayonafasi ya kukata rufaa.
Katika kesi hiyo yenye washtakiwa sita,Mahakama hiyo ilimwachia huru mshitakiwa wa sita Masunga Kashindye ambaye baada ya kuachiwa alitimua mbio na kuelekea kusikojulikana ambapo mshitakiwa wa tano kwenye kesi hiyo Maiko Samweli alifariki dunia wakati akiwa mahabusu .