RC MNYETI AMPA MTIHANI MKANDARASI ANAYEJENGA BARABARA YA MBULU MJINI


Na Beatrice Mosses - Manyara 
Mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti amempa mtihani mkandarasi wa kampuni Mkandalasi Gopro construction Ltd, anayetengeneza barabara ya Mbulu mjini kwa kiwango cha lami. 

Mnyeti amemwambia mkandarasi huyo kuwa iwapo kama atafaulu mtihani wa kutengeneza barabara hiyo ya mita 500 alizopewa kwa kiwango kinachotakiwa yupo tayari kumpa km. 05 zinazotakiwa kutengenezwa mjini hapo ambazo ziliahidiwa na Rais Magufuli. 

Mnyeti ameyasema hayo wakati alipokuwa akikagua barabara hiyo ya mita 500 za mwanzo ambapo kwa sasa ujenzi wake bado unaendelea. 

"Hakikisheni mnamaliza huu mradi mapema na kwa wakati ili niweze kuwaletea fedha zingine sio mradi unakaa, mnakaa, tunaombea fedha zinakuja halafu zinakaa bila kazi inakuwa hakuna mnachokifanya. 

"Sasa tengenezeni kwa kiwango ili mpate kazi nyingine, mkiharibu mimi sitakubali mpate tenda nyingine, mnaweza mkaenda pale Babati yule mkandarasi amefanya kazi ya hatari sana na ndio maana tumemuongeza kazi nyingine. 

"Na nimeagiza TARURA wampe ile lami yote mpaka amalize hata kama watu watakuwa wanalalamika sijui tenda zimekiukwa ni kwa sababu kiwango anachotengeneza pale ni cha kiwango cha juu sana. 

"Sasa bwana mzee tunakupa mtihani huu wa kwanza mita 500 ukitekeleza kwa kiwango cha juu hata tenda hatutatangaza kwa sababu sisi tunataka ubora na hapa kuna km 05 na pesa ipo sisi ni namna tu mnaitumiaje kwa haraka na kwa spidi inayotakiwa", alieleza Mnyeti.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post