BASI LA FREYS COACH LAWAKA MOTO LIKITOKEA SHINYANGA KWENDA TANGA


Na Josephine Charles - Malunde 1 blog
Basi la Freys Coach lenye namba za usajili T119BDY aina ya Scania Bus linalofanya safari zake kutoka Shinyanga kwenda  Tanga limeungua moto katika  eneo la kijiji cha Usanda kata ya Samuye Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga barabara ya Tabora - Shinyanga.


Tukio hilo limetokea leo Ijumaa Oktoba 18,2019 majira ya saa 12 na nusu baada ya kutoka Shinyanga Mjini kuelekea Tanga.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio wanasema basi hilo limeungua matairi mawili ya nyuma upande wa kulia na kwamba hakuna madhara yaliyojitokeza kwa abiria.

Inaelezwa kuwa abiria walishuka na kuanza zoezi la kuzima moto huo kwa maji na mchanga na muda mfupi Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilifika eneo la tukio na kufanikisha kuzima moto huo.



"Tumezima kwa maji na mchanga,zimamoto nao wamefika,gari limezima,hakuna uharibifu wa mali za abiria wala majeruhi,gari halijateketea lote,abiria tumefanya juhudi za kuzima moto,sasa tunasubiri magari mengine kutoka Mwanza ili tuendelee na safari yetu",wamesema abiria wakizungumza na Malunde 1 blog.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao amesema basi hilo lililokuwa na abiria 20 limewaka moto na kusababisha uharibifu wa mali.

"Chanzo cha tukio ni break za basi hilo kung'ang'ania kwenye disk za matairi,hakukuwa na madhara yoyote kwa abiria wa basi hilo",amesema Kamanda Abwao.

Muonekano wa basi la Freys Coach baada ya kuungua leo. Picha zote na Josephine Charles - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post