BENDI YA KITIME, MSONDO NGOMA ZAWASHA MOTO TAMASHA LA 38 BAGAMOYO




Na Andrew Chale, Bagamoyo
MAKUNDI ya muziki wa dansi nchini John Kitime and JFK Band pamoja na kundi l Msondo Ngoma Music band usiku wa Oktoba 24, yamepagawisha mashabiki wake katika tamasha la 38 linaloendelea katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo.

Bendi ya Kitime ilipanda jukwaani na kushangiliwa na idadi kubwa ya mashabiki, nyimbo mbalimbali zilizopigwa na mtaalamu huyo wa muziki, zilikonga nyoyo za mashabiki waliojitokeza ukumbini humo.

John Kitime ambaye pia ni mchambuzi wa muziki wa dansi hapa nchini, katika tamasha hilo alilitawala vilivyo jukwaa kwa kulicharaza gitaa la solo huku akiimba nyimbo za bendi hiyo.

Mwanamuziki huyo alilibamba jukwaa zaidi alipopiga wimbo wa Nyongise uliowahi kutamba na bendi ya Vijana Jazz, nyingine ni Macho yanacheka, Siri ya kwako (Masantula), Nimekusamehe lakini Sitokusahau na Binaadam sina hamu ambao uliwakumbusha mashabiki wa muziki wa miaka iliyopita na pia alirudia nyimbo nyingine zilizowahi kutamba miaka ya nyuma.

Wanamuziki wanaoisaidia zaidi bendi hiyo ni pamoja na Khadija Mnoga ‘Kimobiteli’ ambaye naye alilitawala vilivyo jukwaa.

Mbali ya Kitime katika ukumbi huo, bendi ya muziki wa dansi ya Msondo ilipanda jukwaani na kuanza na wimbo wake wa ‘Ndoa ndoano’ na kufuatiwa na Cheusi Magala ambazo zilisababisha mashabiki kutokukaa kwenye vitini.

Msondo Ngoma mara kadhaa iliingiwa na hitilafu kadhaa kutokana na ‘setting’ ambayo ilisababisha mwanamuziki Abdul Ridhiwani Pangamawe kushindwa kulicharaza gitaa la ‘rithym’.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post