KATIBU WA CHADEMA AONYA VITISHO NA LUGHA ZA MATUSI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA


Mhe. Conchesta Rwamlaza

Na Lydia Lugakila - Malunde 1 blog
Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Kagera Mhe. Conchesta Rwamlaza ambaye pia ni Mbunge viti maalumu amewataka viongozi wa vyama vya siasa mkoani Kagera kuepuka na masuala ya vitisho na lugha zisizofaa katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 24,2019.

Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 16, 2019 amesema kazi ya viongozi ni kuongoza njia hivyo wanapaswa kuwa mfano kwa wananchi wao kwa kuongoza vyema jukumu kwa kujiepusha na masuala yasiyofaa katika jamii ikiwemo vitisho na lugha zisizofaa zinazoweza kubeza harakati na maendeleo ya chama kusonga mbele.

Amesema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 24 ni kipindi ambacho kinawataka viongozi kutoa matokeo chanya katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla. 

"Katika kipindi cha nyuma wapo baadhi ya viongozi walitoa lugha za vitisho. Mimi kama kiongozi wa chama nayakemea madudu yote,viongozi wafuate misingi ya vyama vyao ili kuruhusu suala la maendeleo kuwa juu’’,alisema Rwamlaza.

Aidha amewataka wananchi kuteua kwa haki viongozi watakaokidhi matarajio ya wananchi katika kuwaletea maendeleo. 

Hata hivyo mbunge huyo amepongeza zoezi la uandikishaji kwenye daftari kwa ajili ya  uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuyajali makundi maalumu kwani kwa asilimia kubwa makundi hayo yamehudumiwa ipasavyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post