Picha ya mfano wa daktari
Mahakama ya hakimu mkazi wilaya ya Kigoma imemhukumu kwenda jela miaka miwili na nusu daktari feki ambaye anatajwa kusababisha vifo vya wagonjwa kupitia kazi ya udaktari ikiwemo kufanya upasuaji.
Daktari huyo feki aitwaye Maxmillian Martin amepelekwa mahakamani hapo kwa makosa matano likiwemo la kufoji cheti cha shahada ya kwanza ya udaktari kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam, cheti cha mafunzo kwa vitendo cha hospitali ya rufaa ya Muhimbili, cheti cha chama cha madaktari, kufanya kazi ya udaktari wakati si daktari na kufanya kazi ya udaktari bila leseni.
Inaelezwa alifanya kazi katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu na kulipwa mshahara wa zaidi ya milioni mbili kwa zaidi ya miaka miwili na miongoni mwa mashahidi ambaye alitoa taarifa polisi alieleza alichukua hatua hiyo baada ya kuona vifo vikiongezeka kwa anao wahudumia.
Akisoma mwenendo wa kesi hiyo hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Kigoma Keneth Mutembei amesema, mshtakiwa alikana kuwa vyeti hivyo ni vyake ila alikuwa anafanya kazi kwa kujitolea ili apate ada ya kwenda chuo kwani alishindwa kuendelea na masomo ya udaktari mwaka 2004 na kuwa yeye ni kijana mwenye akili na matokeo ya daraja la nne.
Alipoambiwa kujitetea kabla ya hukumu aliiomba mahakama hiyo kumpa kifungo cha nje kutokana na kutegemewa na familia na watoto wanne na kuwa afya yake si njema hivyo hakimu kuamua mshtakiwa kwenda jela kwa miaka miwili na nusu.
Chanzo - EATV
Chanzo - EATV
Social Plugin