Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema pamoja na afisa utamaduni wa Wilaya Cloude Mpelembwa wameeleza kuwa hawajakataza watu wasifanye ibada katikati ya wiki.
Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya hiyo, baada ya mkuu wa Mkoa wa Dar Paul Makonda kutengua kauli ya awali ya mkuu wa wilaya ya Ilala ya kuwataka wananchi kuto fanya ibada katikati ya wiki.
Mjema amesema kwamba watu wamemtafasiri vibaya kuwa amekataza ibada ila amepinga wale wanao anzisha makanisa yasiyo rasmi.
“Wale ambao wamejenga tu turubai na wameweka maspika hao lazima watuambia wamesha sajiliwa na nimemuagiza afisa utamaduni aende akawaangalie kama wamesajiliwa,” amesema Mjema.
“Nataka niliweke sawa kabisa mimi ni muumini mzuri wa kumuamini Mungu siwezi kuzuia watu wasiende kuabudu tumesema kuna watu wanaanzisha makanisa yasiyo stahili na ukiingia ndani ya makanisa hayo unakuta watu wa tano au sita wanao sali jumatatu hadi jumatatu. Kazi wanafanya lini,” amesema Mjema.
Naye afisa utamaduni wa manispaa hiyo Mpelembwa, amesema mkuu wa wilaya hakuwa na kosa lolote bali alitoa ushauri kuwa matumizi ya vyombo vya mziki visiwe kero kwa wananchi wengine na waumini wanatakiwa wafanye kazi za kujiletea kipato.
“Siku za ibada za msingi kabisa ni Ijumaa, Jumamosi na Jumapili, lakini Jumatatu mpaka Ijumaa watu wanaruhusiwa kufanya ibada katika maeneo ya ibada na ushauri ulitolewa kwamba wazingatie katika matumizi ya vyombo vya muziki," amesema Mpelembwa.