Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KUTOPANGA BAJETI YA FAMILIA CHANZO CHA LISHE DUNI KWA WAJAWAZITO NA WATOTO WACHANGA



Mkurugenzi wa Shirika la wanahabari la Elimisha,Festo Sikagonamo akitoa elimu ya Upangaji wa Bajeti katika ngazi ya familia kwa wanahabari kutoa vituo mbalimbali vya redio vya wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Maafisa kutoka Shirika la wanahabari la Elimisha wakitoa elimu juu ya namna ya kupanga na kuichanganua bajeti katika ngazi ya familia kwa baadhi ya wakazi wa Tukuyu wilayani Rungwe.
Na Joachim Nyambo,Mbeya.

Kukosekana kwa utaratibu wa upangaji bajeti za mwaka ndani ya familia kumetajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa ukosefu wa uhakika wa chakula bora na hivyo kupelekea familia nyingi nchini kuwa na lishe duni.

Hatua ya uwepo wa lishe duni imesababisha familia nyingi kujikuta zikikumbwa na maradhi yatokanayo na ukosefu wa lishe bora kama udumavu na utapiamlo ambayo zaidi yamekuwa yakiwakumba watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.

Takwimu zinaonyesha mikoa ya nyanda za juu kusini ikiwemo mkoa wa Mbeya inakabiliwa na tatizo kubwa la udumavu na utapiamlo licha ya kuwa miongoni mwa maeneo yanayozalisha kwa wingi mazao ya chakula hususani mahindi,maharage,mtama,ndizi na matunda ya aina mbalimbali.

Akizungumzia changamoto hiyo,Mkurugenzi wa Shirika la Wanahabari la Elimisha ambalo hivi sasa linaendesha Mradi wa Utoaji elimu ya Umuhimu wa Upangaji Bajeti ndani ya familia,Festo Sikagonamo amesema jamii mkoani hapa imejikita zaidi kwenye mipango ya kuzalisha lakini haipangi namna nzuri ya kutumia kitakachozalishwa.
Sikagonamo amesema familia nyingi zinakosa kupanga bajeti za mahitaji halisi ikiwemo ya chakula maalumu kinachohitajika wakati mama akiwa mjamzito na pia mtoto anapozaliwa hatua inayosababisha watu hao kulazimishwa kula chakula chochote kitakachopatikana pasipo familia kujali uhitaji maalumu walio nao.

“Kama familia husika ingepanga bajeti kuwa kwakuwa kuanzia mwezi flani katika mwaka husika mama atakuwa mjamzito basi ingempangia pia mahitaji yake ya chakula yatagharimu kiasi gani kwakuwa failia hii pia itajua kuwa kwa wakati huo atahitaji chakula cha aina ipi.Vivyo hivyo kwa mtoto atakayezaliwa,inapaswa kujua huyu akija atahitaji chakula gani na wakati huo huo ikiendelea kumgharamia mama anayemnyonyesha mtoto huyu mchanga kwakuwa bajeti ilipangwa toka awali.”

“Lakini sasa utakuta haikupangwa bajeti juu ya mama akiwa mjamzito,wakati ananyonyesha baada ya kujifungua na inakuja kumkumba hadi mtoto tangu wakati anahitaji maziwa ya mama pekee na hata anapoanza kula vyakula vingine.Hapo ndipo unakuta kwakufa familia imepika makande basi  na mtoto atatafuniwa ili ilishwe makande.Kwakuwa zimepikwa ndizi basin aye analazimika wampondee alishwe pasipo kujali umri na mahitaji yake halisi ni yapi.”amesema Sikagonamo.

Mkurugenzi huyo amesema iwapo jamii itabadilika na kuweka misingi ya kupanga bajeti itasaidia familia nyingi kuondokana na tatizo la lishe duni kwakuwa gharama zote zitakuwa zimeainishwa tokea awali sambamba na vyanzo vya mapato vitakavyoiwezesha familia kuzalisha kinachohitajika na hata ziada.

“Kila sehemu tunakokwenda unapowauliza watu kumi iwapo familia zao zinao utaratibu wa kupanga bajeti za mwaka mara nyingi tunakosa hata mkono wa mtu mmoja aliyenyoosha.Hii inaonesha jambo hili halifanyiki kabisa kwenye familia zetu.Sasa tukiendelea na mfumo huu ni wazi kuwa tutazidi kuwa na matatizo mengi yakiwemo haya ya lishe duni.Maana kama Familia haijui inahitaji kiasi gani cha chakula kwa mwaka itashindwa pia kujua izalishe na itunze kiasi gani.”amesema.

Amesema pia upangaji huo wa bajeti za mwaka unaweza kuzisaidia familia nyingi kuwa na uhifadhi sahihi wa mazao wanayozalisha na kuuza ziada pekee tofauti na sasa ambapo watu wengi wamekuwa wanazalisha chakula kingi lakini kwakuwa hawajui mahitaji halisi ya familia hutapanya hovyo na muda mfupi kujikuta hawana tena chakula na hapo ndipo inabidi kila mwanafamilia kula kile kilichopatikana na kuyaumiza makundi yaliyo na mahitaji maluumu hasa wajawazito na watoto wadogo.

Uchunguzi pia uliofanywa na Mtandao huu,umebaini familia nyingi kuishi kwa mazoea katika maisha ya siku zote hatua inayopelekea hata kutokuwepo kwa mpango sahihi wa kujadili masuala ya uzazi ikiwemo lini wazazi watafute mtoto mpya na hivyo mimba nyingi kuonekana kutungwa kwa bahati mbaya.

Hali hiyo inaonekana kusababisha familia kushindwa kuwa na wakati rafiki wa kuwatunza watoto wanaozaliwa kwa mfumo huu kwakuwa yanakosekana pia maandalizi rafiki ambayo yangewezesha mtoto husika kuishi kwa kupata mahitaji stahiki kama vile wazazi wangepanga na kutarajia ujio wake.

Baadhi ya wakazi jijini Mbeya wanasema ni jambo lisilowahi kutokea kwenye familia zao tangu wangali wadogo kukalishwa na wazai au walezi wao na kupanga au kuichambua bajeti kwa pamoja.Hivyo hata linapozungumzwa suala la bajeti yenye kulenga lishe bora ndani ya familia linaonekana jambo geni kwao.

“Kwangu mimi hata nyumbani kwangu haijawahi kutokea eti tumekaa na mume wangu tukapanga bajeti ya mwaka unaofuata.Kwanza ni jambo ambalo haliwezekani.Nadhani ni kwakuwa kwanza kipato change tu ni cha kuungaunga sina uhakika nacho.”Amesema Rouse Mourice mama wa familia ya watoto wawili.

Mkazi mwingine Nancy Mwandumbya anasema hakuwahi kuwaza kupanga bajeti.Kinachofanyika ndani ya familia yake katika suala la ununuzi wa vyakula ni kununua kile kinachohitajika kuliwa siku hiyo hasa kwenye suala la kitoweo.

“Kwakweli kwangu ni swali gumu ukiniuliza kipato change kwa mwaka ni shilingi ngapi au matumizi kwa mwaka.Vitu vichache tu ninavyoweza kukisia kuwa huenda kwa mwaka tunatumia kiasi gani.Hivi ni mchele labda na mafuta ya kula.Navyo ni vigumu kusema vinagharimi kiasi gani mpaka tukatenga bajeti.Ndivyo ilivyo kwa familia nyingi za sisi wahangaikaji.Sasa unaweza kuona bajeti ya wajawazito inaandaliwaje kwenye familia kama hizi.”amesema Nancy.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com