WAITARA ATAKA VIONGOZI KUTOA TAARIFA KWA WAZAZI KUCHANGIA MICHANGO SHULENI



Naibu Waziri Ofisi ya Rais (TAMISEMI ) anayesimamia Sekta ya Elimu Mhe. Mwita Waitara

Na Lydia Lugakila - Malunde 1 blog Kagera
Naibu Waziri Ofisi ya Rais (TAMISEMI ) anayesimamia Sekta ya Elimu Mhe. Mwita Waitara amewaagiza viongozi mbalimbali nchini kupitia bodi za shule,kamati za shule, vikao vya wazazi ,mabaraza na mikutano ya hadhara kutoa taarifa kwa wazazi kuchangia baadhi ya michango ya watoto wao shuleni kwa mpango mahususi ili kukuza sekta ya elimu nchini.

Naibu Waziri Mwita Waitara ametoa agizo hilo leo Oktoba 16, 2019 wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Kagera katika ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua miradi ya elimu sambamba na kuongea na watumishi mkoani Kagera

Agizo hilo la Mhe. Mwita kwa viongozi mbalimbali na wadau wa elimu nchini juu ya utoaji taarifa kwa wazazi kuhusu kuchangia ya michango ya watoto wao shuleni kwa mpango mahususi limekuja baada ya kusomewa taarifa fupi na Afisa Elimu Mkoa wa Kagera Juma Mhina kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa huo Profesa Faustin Kamuzora iliyoelezea hali ya elimu katika mkoa huo zikiwemo changamoto na ufaulu wa mtihani wa darasa la saba mwaka 2019.

Afisa Elimu mkoa wa Kagera Juma Mhina amesema licha ya juhudi kubwa za Rais Magufuli katika utoaji elimu bila malipo changamoto nyingi zimeendelea kuwepo katika sekta hiyo kwani kuna baadhi ya wazazi wamekuwa hawawezi kujitoa kikamilifu katika kushirikiana na serikali katika kuchangia baadhi ya michango ya maendeleo ya watoto wao shuleni.

Katika taarifa hiyo Mhina amesema mkoa huo umefanikiwa pa kubwa katika baadhi ya masuala ikiwemo la uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya awali na darasa la kwanza ambapo katika elimu ya awali wameandikisha wanafunzi kwa asilimia 97 na darasa la kwanza kwa asilimia mia moja na nane 

Afisa elimu  amesema miongoni mwa changamoto zilizopo kuwa ni pamoja upungufu wa madawati 48,509 kwa shule za msingi 48 elfu 509, upungufu wa madawati katika shule za sekondari 17,000 vyumba vya madarasa , upungufu wa walimu wa sekondari kwa upande wa masomo ya sanaa ambao ni 48,000 ambapo kwa masomo ya sayansi ni 1060 huku akitaja upungufu wa walimu upande wa elimu msingi kufikia 6,571. 

Akiipokea taarifa hiyo Naibu Waziri huyo ameupongeza mkoa huo kwa ufaulu mzuri wa matokeo ya darasa la saba kwa kushika nafasi ya 4 kitaifa kwa ufaulu wa 88.11% ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo ulishika nafasi ya 5.

Naibu Waziri huyo amesema kuwa wazazi wanapaswa kutambua kuwa serikali ila ilizuia kitendo cha walimu kujikita kuchangisha fedha kwa watoto ambao hawana fedha na kusababisha watoto hao kujengewa chuki.

"Katika hali ya kawaida serikali haiwezi kufanya kila kitu viongozi mbali mbali wadau wa elimu Viongozi wa elimu hakikisheni mnatoa taarifa kwa wazazi kuchangia baadhi ya maendeleo ya shule, viongozi wa shule wanapotoa maelezo kuwa kuna baadhi ya vitu ambavyo huhitaji kuchangiwa,baadhi ya wazazi ambao hawaungi mkono juhudi hizo.

Kuna changamoto ambazo wazazi viongozi wanatakiwa kuchangia kwa kushirikiana na serikali ili kufanikisha sekta ya Elimu kusonga mbele’’,alisema Waitara.

Amesema ili ufaulu uendelee kuwepo ni lazima watoto wapate chakula shuleni jambo ambalo baadhi ya wazazi hawataki kuchangia 

"Wazazi wamekuwa wakishangilia mahafali kuliko kuchangia maendeleo ya mtoto shuleni, mkoa wa Njombe umefanya vizuri katika uchangiaji wa chakula shuleni",alisema.

Adha alieleza kuridhika na Usimamizi wa miradi ya elimu mkoani Kagera na kuwa tayari serikali imetenga shilingi bilioni 12 na laki 5 kukamilisha kila boma kwa kiwango walichokubaliana huku akiwahimiza Viongozi nchini kusimamia vizuri fedha zinazokuja ili ziweze kutoa matokeo chanya na kuwa serikali inatarajia kumaliza changamoto ya upungufu wa walimu mwaka huu

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti amemhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa atahakikisha wananchi wanashirikiana katika kuchangia maendeleo ya shule ili kuongeza ufaulu mkoani Kagera.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post