Kushoto ni Afisa Mwandikishaji daftari la kudumu la wapiga kura akiandika taarifa za Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti aliyefika katika uwanja wa Ndege Manispaa ya Bukoba kuboresha taarifa zake
Na Lydia Lugakila- Malunde 1 blog
Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti amesema hayuko tayari kumvumilia mtu au kundi la watu litakalosababisha changamoto katika zoezi la kuboresha daftari la kudumu la mpiga kura kutokana na serikali kuwekeza fedha nyingi ili kuhakikisha wananchi wake wanapata fursa hiyo na wanatumia haki yao kikatiba kupata viongozi wanaohitaji kwa maendeleo ya taifa.
Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti ametoa kauli hiyo leo Oktoba 4, 2019 wakati akikagua hali halisi ya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura linaloendelea katika zahanati ya Kashai iliyopo Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.
Jenerali Marco Elisha Gaguti amesema kila Mtanzania anatakiwa awe mlinzi wa taifa la Tanzania na kuwa hakuna kuruhusu kwa njia yoyote ile kuwapenyeza watu ambao hawana sifa za msingi za kujiandikisha katika Daftari la kudumu la mpiga kura.
Aliwataka viongozi wa vyama vya siasa,watendaji na wananchi mkoani Kagera kuweka umakini wa kipekee katika wilaya zote za mpakani ikiwemo Misenyi, Kyerwa, Ngara, Karagwe kuhakikisha kwamba hakuna mtu asiye na sifa anajipenyeza kujiandikisha katika daftari hilo.
"Viongozi wa vyama vya siasa ,watendaji na wananchi kila mtu kwa nafasi yake ahakikishe kwamba wale wanaojiandikisha au kufanya maboresho ya kumbukumbu zao ni wale tu wenye sifa za msingi’’,alisema Brigedia Gaguti
Aidha amefurahia muitikio mzuri wa wananchi wanaojitokeza katika uboreshaji wa daftri hilo na kutoa wito kwa wananchi wote katika maeneo yote ambayo yamewekwa vituo hivyo vya maboresho ya taarifa kutumia muda huo vizuri kuhakikisha wote wenye sifa za msingi za kupiga kura wafanye uboreshaji wa taarifa zao ili waweze kustahili kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao 2020.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera pia amefanya uboreshaji wa kumbukumbu zake katika kituo cha kujiandikisha kilichopo katika uwanja wa Ndege Manispaa ya Bukoba na kuwahimiza wananchi mkoani Kagera kutumia siku 7 za uboreshaji daftari la wapiga kura Oktoba 3 hadi Oktoba 9 kuhakikisha wamejiandikisha.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti akiboresha taarifa zake kwenye daftari la kudumu la wapiga kura katika uwanja wa Ndege Manispaa ya Bukoba
Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti akiwa eneo la zahanati ya Kashai kukagua zoezi la uboreshaji daftari la wapiga kura
Social Plugin