Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JESHI LA POLISI DODOMA LAKANUSHA KUMPIGA MWANANCHI

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.

Jeshi la Polisi mkoa wa Dodoma limekanusha kuhusika na  taarifa za kumpiga Raia mmoja ajulikanaye kwa jina la   Elisha Hezron Wanjara[39] na kudai kuwa taarifa hizo sio za kweli na zimerushwa na Baadhi ya Vyombo vya Habari bila kufanyiwa uchunguzi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Girres Muroto amesema Tarehe 7,oktoba ,2019 Mwandishi wa Habari kupitia GLOBAL TV ONLINE ,Bw.Mohamed Zengwa alirusha katika mitandao ya kijamii habari ya mtu mmoja aitwaye ELISHA HEZRON WANJARA[39]MJITA Fundi Ujenzi wa Barabara katika kampuni ya STECOL inayofanya kazi za ujenzi hapa Dodoma  ambapo taarifa hizo zilidai mtu huyo alipigwa na Jeshi la Polisi.

Kamanda Muroto amesema katika taarifa hiyo ilifafanua kuwa Bw.WANJARA alipigwa na askari polisi wa doria na kuporwa simu pamoja na fedha kiasi cha Tsh.Elfu 70 na kupakiwa kwenye gari la polisi na kuwekwa kwenye mahabusu ya Polisi  na baadaye kuachiliwa huru bila matibabu,bila kurejeshewa simu na pesa zake  na alikwenda kwa mkuu wa wilaya na kuongea naye juu ya jambo hilo na kurusha mtandaoni.

Hata hivyo,Kamanda Muroto amesema habari hiyo ni ya uongo na haina ukweli wowote  hivyo Bw.WANJARA alisema  uongo ,hakuibiwa simu ,hakuporwa fedha wala kupigwa na askari  kama alivyojieleza kwa mwandishi wa habari mbele ya mkuu wa wilaya wa  Dodoma mjini.

Aidha,Kamanda Muroto ameelezea Ukweli wa tukio kuwa ,siku ya Tarehe 6/10/2019  Bw.Elisha Hezron Wanjara na Mwenzake mmoja aliyejulikana kwa jina la utani NGINJANGINJA walikwenda nyumbani kwa Paulo Mkazi wa Mtaa wa IPAGALA akitafuta chumba cha kupanga na walimchukua mwenyeji wao wakaenda kunywa pombe za kienyeji nyumbani kwa mama Eliza.

Kamanda Muroto ameendelea kufafanua kuwa ,wakati wanaendelea kunywa pombe ,Bw.WANJARA alimpatia Simu Bw.PAULO CHIPAGALA awapige picha na aliwapiga picha mbalimbali wakati wanakunywa pombe na baada ya kulewa walianzisha ugomvi mkubwa  na kupigana kwa muda mrefu.

Hivyo,waliumizana na wote wakasambaratika eneo hilo  na haikujulikana kila mmoja alikokwenda  na simu aliendelea kubaki nayo PAULO CHIPAGA  aliyepewa na mwenye simu kabla ya kulewa na kupigana.

Kamanda Muroto amebainisha ,usiku wa saa 3:45 Elisha Wanjara aliokotwa na wapita njia na kumpeleka kituo cha polisi  Central Dodoma akiwa amelewa pombe ,hajitambui na ana majeraha ya kupigwa  na aliandikiwa PF3 ili aende kutibiwa  na waliompeleka ni watu walewale waliomleta kituoni.

Baada ya kurudisha PF3 aliyopewa kituo  cha Polisi ,kulipopambazuka alikwenda kwa mkuu wa wilaya ya Dodoma ,akatoa taarifa na maelezo ya uongo kuhusu jeshi la polisi akisingizia askari kumpiga ,kupora simu na fedha.

Kamanda Muroto amevieleza vyombo vya habari kuwa,Jeshi la polisi limefanya uchunguzi kuhusu tukio hilo  na kubaini ukweli na mafanikio ambayo ni Bw.WANJARA hakukamatwa na askari polisi kwenye msako,simu haikuporwa,bali alimpatia PAULO CHIPAGA na ilipatikana kutoka kwa CHIPAGA,Majeraha aliyopigwa ni kutokana ugomvi wake na mwenzake.

Mambo mengine yaliyobainishwa na Jeshi la polisi kuwa ni hakuporwa Tsh.70,000,na siku ya tukio aliomba Tsh.5000 kutoka kwa JOHN NTALE Msimamizi wake wa kazi,amewasingizia askari polisi na kutoa maelezo ya uongo kwa mkuu wa Wilaya  na kuudanganya umma wa Tanzania na kulichafulia jeshi la Polisi kwa tukio la kuunda na Maneno ya uongo.

Kwa upande wake Bw.WANJARA amehojiwa na amekiri kuwa alitoa taarifa za uongo na alikuwa amelewa pombe.

Kutokana na tukio hilo,mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi la polisi na amefunguliwa mashtaka kwa kutoa taarifa za uongo  na atafikishwa mahakamani hivyo kamanda Muroto ametoa onyo kwa wanaotumia vibaya ofisi za serikali kutoa taarifa za uongo  na kuwataka wanahabari kuzifanyia uchunguzi na subira habari kabla ya kuzirusha ili kuondoa mkanganyiko katika jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com