JIJI LA DODOMA LATOZWA FAINI KUTOKANA NA UCHAFU WA MACHINJIO

Na Lulu Mussa
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) hii leo imefunga machinjio ndogo ya Msalato kwa muda usiojulikana na kupiga faini kwa kosa la kukithiri kwa uchafu wa mazingira na miundombinu chakavu.
Hatua hiyo imefikiwa mara baada ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kufanya ziara ya kushtukiza katika eneo hilo na kujionea Mazingira yasiyoridhisha kwa usalama wa afya za binadamu. 
Katika ziara hiyo, wabunge wamejionea mazingira yasiyoridhisha na kuhatarisha afya za watumiaji wa nyama inayochinjwa machinjioni hapo ikiwa ni pamoja na kurundikana kwa samadi, kukithiri kwa harufu kali na kukosekana kwa maji safi.
Bw. Gratius Mwesiga, Afisa Mifugo wa Jiji la Dodoma ameieleza Kamati hiyo kuwa ukarabati katika eneo hilo umeanza na unaendelea kwa awamu, ikiwa ni pamoja na ukarabati wa mifumo ya maji taka.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mussa Sima amesema lazima hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa manufaa ya afya za walaji. "Sisi watu wa Mazingira afya za binadamu ni kipaumbele namba moja, hali hii haikubaliki" Sima alisisitiza. 
Waziri Sima amemuagiza Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Nchini (NEMC) Dkt. Samwel Gwamaka kufanya tathmini ya haraka na kina na kuhakikisha kuwa machinjio yanazingatia taratibu zilizopo katika Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira Kanali Mstaafu Masoud Ali amesema hali ya usafi katika machinjio hiyo haidhirishi na kuwataka NEMC kuchukua hatua. "NEMC msingechukua hatua, sisi Kamati tungechukua, haiwezekani hali hii haikubaliki" Alisisitiza Mhe. Masoud Ali.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC amelitoza faini Jiji la Dodoma ya kiasi cha Shilingi Milioni tano (5) kwa mujibu wa kifungu namba 194 cha sheria ya usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na kutakiwa kuilipa ndani ya wiki mbili.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post