DC MWEGELO : CHAGUENI VIONGOZI WA KUENDANA NA KASI YA RAIS MAGUFULI


Mhe. Joketi Mwegelo 

Na Shushu Joel
Mkuu wa wilaya ya Kisarawe ambaye anakaimu Ukuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Joketi Mwegelo amewataka wananchi wa Halmashauri ya Chalinze kuwachagua viongozi wenye utayari na uwezo wa kuendana na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Rai hiyo ameitoa wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Bwilingu kwenye viwanja vya kituo cha mabasi cha Barabara ya Morogoro.

Mkuu huyo wa wilaya aliwakumbusha na kuwasisitiza wananchi hao kutambua dhamana kubwa waliyonayo na yupi ni kiongozi atakayekuwa ni kiungo kikubwa kwa viongozi wa juu na anayeweza kuendana na utendaji wa Rais Magufuli.

Pia Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kuendelea kujitokeza kwenye zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la kupiga kura huku akiwapa msisitizo kuwa ni wale watakaokuwa kwenye orodha ndani ya daftari la wapiga kura tu ambao watapata fursa ya kupiga kura.

 "Wananchi wenzangu wale ambao wanadhani kuwa kile kitambulisho cha kupiga kura kitawawezesha kushiriki uchaguzi huu, hapana. Uchaguzi huu tunatumia daftari hivyo ni muhimu kwenda kujiandikisha".

"Jambo la kuwa na vitambulisho kuwa kigezo si kweli bali ni wewe tu kuweza kufika kituoni na inakuchukua dakika 2 tu",alisema.

Katika hatua nyingine,Mhe, Mwegelo amempongeza Mbunge wa jimbo la  Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete kwa utekelezaji na ufanikishaji wa miradi mbalimbali katika jimbo lake na jinsi alivyojitokeza yeye akishirikiana na wananchi kuhamasisha uandikishaji.

Aidha amewataka wananchi hao kuwa na viongozi watakaochaguliwa kwenye vitongoji na vijiji wawe wachapakazi kwa ajili ya kufanya kazi nzuri ya kuleta maendeleo.

"Ninyi wenyewe mashuhuda na Mbunge ameeleza jinsi Miradi mikubwa kama ya maji,afya,madarasa, miundombinu na umeme ilivyotekelezwa kwa asilimia kubwa sana. Nakupongeza Mhe. Mbunge kwa utekelezaji mzuri wa majukumu",alisema.

Naye mzee Zaidi Lufunga (78) akizungumza kwa niaba ya Wana Chalinze amempongeza mkuu huyo wa wilaya kwa kujionea mafanikio makubwa yaliyofanywa na serikali ya awamu ya tano katika jimbo la Chalinze.

"Miaka yetu changamoto zilikuwa nyingi sana, lakini kipindi hiki cha Rais Magufuli kwa kushirikiana na mbunge wetu Ridhiwani Kikwete mafanikio tunayapata na kazi nzuri inaonekana. Kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa na iliyokuwa ndiyo ndoto zao ni tu tutachagua viongozi wenye hofu ya Mungu",alisema Mzee Lufunga.

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete amempongeza mkuu huyo wa wilaya kwa ujio wake wa kujionea jinsi Wanachalinze wanavyojitokeza katika zoezi la kujiandikisha.

Amewapongeza wakazi wa kata ya Bwilingu kwa kujitokeza kwa wingi ili kumsikiliza mkuu wa wilaya akieleza kuwa hilo ni jambo kubwa na kwa hakika linatoa dalili kuwa wananchi wako tayari. 

Hadi kufikia jana Halmashauri ya Chalinze ilikuwa imefikia Asilimia 74 ya Uandikishaji na baada ya kukatika kwa mvua kumekuwa na wingi wa wananchi kujiandikisha. Zoezi hili linatarajiwa kuisha tarehe 17 Oktoba ambapo matarajio ya kuandikisha watu 136,000 utafikiwa huku hadi jana watu zaidi ya 90,000 wakiwa wamejitokeza kujiandikisha.


Mbunge wa jimbo la Chalinze Mhe, Ridhiwani Kikwete akizungumza na wakazi Bwilingu juu ya kujiandikisha kwenye daftari la kupiga kura.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post