KIJANA ALIYEISHI KWA KUPUMULIA MASHINE AFARIKI DUNIA


Hamad Awadh, aliyeishi kwa kutegemea mashine ya kumsaidia kupumua amefariki dunia jana jioni Oktoba 17, 2019 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu.

Mke wa Awadh aitwaye Catherine Kulekana amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kusema, hali ya mumewe ilianza kubadilika usiku wa kuamkia jana akawa chini ya uangalizi wa madaktari hospitalini hapo. Ilipofika asubuhi hali yake haikurejea kawaida na saa 10 jioni alifariki.

Juni 10, 2019 Mloganzila ilimpa msaada wa mashine hiyo ya kumsaidia kupumua yenye thamani ya Sh4 milioni kutokana na matatizo yake ya afya ambayo yalimlazimu kutumia mashine ya Oksjeni muda wote ili aweze kupumua. Awadh alifikishwa Mloganzila Julai 9, 2018 na kuruhusiwa Juni 9, 2019 baada ya afya yake kuimarika.

Licha ya kutakiwa kurejea hospitali kila baada ya muda alishindwa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutokuwa na usafiri wa kutoka nyumbani kwake Kipawa hadi katika hospitali hiyo umbali wa zaidi ya kilomita 10.

Wadau na taasisi mbalimbali walijitokeza kumsaidia ikiwa ni pamoja na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) lililomfungia umeme katika nyumba aliyokuwa akiishi na kumpatia Sh10 milioni za matibabu. Awadh aliomba msaada Tanesco kutokana na mashine ya kumsaidia kupumua kutumia umeme mwingi.

Pia, Hospitali ya Mloganzila ilitoa gari la wagonjwa kwa ajili ya kumpeleka Awadh katika hospitali hiyo kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake, mara ya mwisho hali yake ilibadilika na kulazwa hadi umauti ulipomkuta.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post