Mkuu wa Shule ya Sekondari ya St. Catherine's iliyopo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Fokas Mjema akizungumza Oktoba 5, 2019 kwenye mahafali ya tano ya shule hiyo. Mgeni rasmi alikuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Dkt. Allan Kijazi. (Picha na Yusuph Mussa).
Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Dkt. Allan Kijazi alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya tano ya Shule ya Sekondari ya St. Catherine's iliyopo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Oktoba 5, 2019. (Picha na Yusuph Mussa).
Na Yusuph Mussa, Lushoto
KAMISHNA wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Dkt. Allan Kijazi amesema kuanzishwa kwa Shule ya Sekondari ya St. Cathetine's iliyopo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga kutawasaidia watoto wa kike kupata elimu, sio kwa wilaya hiyo pekee, bali Taifa zima la Tanzania.
Aliyasema hayo Oktoba 5, 2019 alipoalikwa kuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya tano ya kidato cha nne ya shule hiyo iliyopo kwenye viunga vya Mji wa Lushoto nakusema anaunga mkono mawazo ya muanzilishi wa shule hiyo Mtawa Gaspara Kashamba ambaye kwa sasa ndiyo Mkuu wa Masista wa Usambara (COLU) chini ya Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga, ambapo Makao Makuu yao yapo Kwamndolwa wilayani Korogwe.
"Nashukuru mawazo ya Sista Gaspara Kashamba kwa kuanzisha shule hii. Hakika atawasaidia watoto wengi wa kike kupata elimu, sio kwa Lushoto tu bali Taifa zima litafaidika. Hivyo naahidi kumuunga mkono kwa nguvu zangu zote kuhakikisha taasisi hii anaikuza na kuwa chachu ya maendeleo nchini" alisema Dkt. Kijazi.
Dkt. Kijazi aliwataka wanafunzi kujali na kuthamini mchango wa wazazi wao kwa kufanya vizuri kwenye masomo, kwani wazazi wao wanahaha usiku kucha ni namna gani watoto wao watapata elimu nzuri, hivyo katika kulipa fadhila hizo, anataka kuona wanafunzi wote 33 kidato cha nne kwenye shule hiyo wanapata daraja la kwanza.
"Moja ya jambo ambalo mnatakiwa kuwatendea wazazi, na ninyi kufika salama kwenye safari yenu ya maisha ni kufanya vizuri kwenye mitihani yenu kwa ninyi wote kupata division one (daraja la kwanza). Nitafuatilia kuona ndoto zenu zinatimia baada ya wote kuniahidi mtafanya vizuri" alisema Dkt. Kijazi.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo Frank Maduga, ambaye ni Meneja wa NSSF mstaafu wa Mikoa ya Arusha na Tanga, alisema kila siku wanaongeza miundombinu kuona shule hiyo changa inapata mafanikio, na kukiri kwa taaluma si haba, kwani wanafunzi wanaosoma hapo wanajitahidi kufanya vizuri mwaka hadi mwaka.
Akisoma risala yake kwa mgeni rasmi, Mkuu wa Shule hiyo Fokas Mjema alisema shule hiyo iliyoanzishwa Januari 12, 2012 na Mtawa Gaspara Kashamba ikiwa na wanafunzi 29 na walimu sita, ilitokana na maombi ya wazazi, kwani tayari alikuwa ana Shule ya Awali na Msingi ya St. Chatherine's, hivyo wazazi wakataka na sekondari iwepo.
"Mama Gaspara Kashamba kama mdau wa elimu, mpenda maendeleo na mkereketwa wa elimu, akaanzisha O-Level (kidato cha kwanza hadi cha nne) hapa mwaka 2012. Na mwaka jana 2018 alianzisha A-Level (kidato cha tano na sita) kwa combination (mchepuo) za PCM, PCB na HGL. Leo shule ina wanafunzi 272. Lengo la mwanzilishi wa shule hii ni kumwelimisha mwanamke apate elimu bora ya kumfanya akubalike katika jamii.
"Na lengo letu tunaofanya kazi kwa sasa ni pamoja na kufanya St. Catherine's kutoa elimu bora kwa mtoto wa kike, kuifanya shule yetu kuwa miongoni mwa shule bora kitaifa, kutengeneza mabinti ambao wameiva kitaaluma, kiakili, kiroho na kimaadili, kuhakikisha kwamba ufaulu wa shule yetu unaongezeka siku hadi siku ili wanafunzi wetu wafaulu kwa daraja la kwanza na la pili tu, ili wale wa kidato cha nne wajiunge na kidato cha tano, na wale wanaohitimu kidato cha sita, waweze kujiunga na vyuo vikuu vizuri hapa nchini na nje ya nchi",alisema Mtawa Mjema.
Mjema ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Masista wa Usambara (COLU), alisema tangu shule hiyo ilipoanza kufaulisha mwaka 2015, wanafunzi watano walipata ufaulu wa daraja la kwanza, 19 daraja la pili, watano daraja la tatu, na hakukuwa na daraja la nne wala sifuri, huku wakishika nafasi ya kwanza kimkoa kati ya shule 74, na nafasi ya 42 kitaifa kati ya shule 1,162.
Mwaka 2016 daraja la kwanza wanne (4), la pili 12, la tatu 13 na wawili daraja la nne, na kuwa shule ya tatu kimkoa kati ya 99 na 63 kati 1,439 kitaifa. Mwaka 2017 daraja la kwanza wawili, la pili 17, la tatu saba. Nafasi ya pili kimkoa kati ya shule 133, na ya 36 kitaifa kati ya 1,738.
"Mwaka 2018 wanafunzi watano walipata daraja la kwanza, wanafunzi 27 daraja la pili, wanane (8) daraja la tatu na mmoja daraja la nne. Tulishika nafasi ya nane (8) kimkoa kati ya shule 188, na nafasi ya 188 kati ya shule 3,488 kitaifa" alisema Mtawa Mjema.