Viongozi 9 wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe wanatarajia kuanza kujitetea kwa siku tatu mfululizo kuanzia November 4, 5 na 8, 2019 katika kesi ya uchochezi inayowakabili Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hatua ya viongozi hao wanaokabiliwa na Kesi ya jinai namba 112 ya 2018 inatokana na uamuzi mdogo uliotolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambapo katika uamuzi huo Viongozi wa CHADEMA wamewakilishwa na Wakili, Jeremiah Mtobesya na Hekima Mwasipu, huku upande wa Serikali ukiwakilishwa na Wakili Faraja Nchimbi, Wankyo Simon na Salim Msemo.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Simba amesema wiki tatu zilizoombwa na upande wa utetezi ni nyingi hivyo amewapatia wiki mbili ili waweze kuwaanda washtakiwa waanze kujitetea kabla ya mashahidi wao na kusema mashahidi katika kesi hiyo mbali na washtakiwa ni wengi na wanafikia 200, hivyo upande wa utetezi wanahitaji kupewa muda wa maandalizi.
Pia Hakimu Simba amesema kuhusu kielelezo namba 5 ambacho ni video ya maandamano kilichoombwa na upande wa utetezi ili Wataalamu wao wakichunguze kwa sababu wana wasiwasi kimehaririwa, watakitumia kupitia vifaa vya mahakama kama vilivyotumiwa na upande wa mashtaka.