Korea Kaskazini imeionya Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kwamba iwapo wataliibua suala la majaribio yake ya makombora kwenye mkutano wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa inawezekana hatua hiyo ikaongeza zaidi nia yake ya kulinda uhuru wa taifa hilo.
Mataifa 15 wanachama wa baraza hilo wanatarajiwa kukutana katika kikao cha ndani hii leo baada ya Korea Kaskazini wiki iliyopita kufyatua kombora jipya linaloweza kurushwa kutokea kwenye nyambizi.
Majadiliano hayo yanafuatia ombi la Ujerumani, Uingereza na Ufaransa.
Alipoulizwa kuhusiana na namna watakavyoulinda uhuru wa taifa hilo balozi wa Korea Kaskazini kwenye Umoja huo Kim Song amewaambia waandishi waendelee kufuatilia kwa makini kuona kile watakachokifanya huko mbeleni na kuongeza kuwa hiyo haimaanishi watafyatua kombora jingine.
Pyongyang inatoa onyo hilo ikiamini kwamba Marekani iko nyuma ya vuguvugu hilo.
Social Plugin