DC MAHUNDI AZITAKA TAASISI ZINAZOHITAJI KUTOA ELIMU YA MPIGA KURA ZIOMBE KIBALI


Mkuu wa wilaya ya Chunya, Mhandisi MaryPrisca Mahundi.

Na Esther Macha - Malunde 1 blog

Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mkuu wa wilaya ya Chunya, Mhandisi MaryPrisca Mahundi amezitaka taasisi zisizokuwa za kiserikali zinazohitaji kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi kuomba kibali kwa Katibu Mkuu wa Wizara mwenye dhamana ya serikali za mitaa. 

Mkuu huyo wa wilaya alisema hayo jana wakati akizungumza na kamati ya ulinzi na usalama wilaya, viongozi wa dini,watalaamu mbalimbali wakiongozwa na mkurugenzi wa halmashauri pamoja ,msimamizi msaidizi na msimamizi mkuu wa uchaguzi wilaya ya Chunya 

Mkuu huyo wa wilaya alisema katika mwongozo huo wa elimu ya mpiga kura kutakuwa na mwongozo wa elimu ulioandaliwa na ofisi ya Rais Tamisemi.

Mhandisi Mahundi alisema lengo la kikao hicho ni maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotaraji kufanyika mwezi Novemba mwaka huu. 

Aidha mkuu huyo wa wilaya alivitaka vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi kuwaelimisha wanachama wao kuheshimu kanuni na taratibu za uchaguzi wa serikali za mitaa zilizowekwa ili kuepuka vurugu. 

"Tunafanya hivi katika halmashauri yetu ili mambo yetu yaweze kwenda vizuri kabisa",alisema mkuu huyo wa Wilaya. 

Aliongeza kuwa kila chama cha siasa lazima kizingatie ratiba za mikutano ya kampeni ili kuondoa migongano isiyo ya lazima wakati kampeni zikiendelea. 

"Lakini pia kwa nafasi yangu nitajitahidi kusimamia vizuri uchaguzi huu wa serikali za mitaa katika wilaya ya chunya ili tuweze Kupata viongozi bora ambao watakuwa chachu ya maendeleo na kuweza kuwa viongozi wenye haki na wajibu",alisema Mhandisi Mahundi. 

Mkuu huyo wa wilaya alisema wilaya ya Chunya ina vijiji 43 na vitongoji 233.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post