Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Mbunge wa jimbo la Mtera mkoani Dodoma Livingstone Lusinde amewataka vijana kote nchini kujitathimini na kuachana na masuala ya anasa ikiwa ni pamoja na Umalaya na badala yake wawajibike katika kazi za kuwaletea maendeleo.
Mhe.Lusinde amesema hayo jijini Dodoma akiwa mgeni Rasmi katika kongamano la Vijana Mkoa wa Dodoma lililolenga kujadili mchango wa Baba wa Taifa Mwl.Julus Kambarage Nyerere ikiwa taifa la Tanzania likifanya kumbukizi ya Miaka 20 tangu afariki dunia mwaka 1999.
Mbunge huyo amesema vijana wa siku hizi wamekuwa wakifanya masuala ya Umalaya na ukahaba na mambo mengine ya anasa wakiwa wadogo na kushinda baa badala ya kuwajibika katika kazi hivyo wanapaswa kubadilika.
“Kijana Mdogo,una miaka 22,huna kazi ya uhakika,huna mshahara lakini una mademu wanne ,wewe ni tatizo,shida ni wewe,piga hela zote ulizotoa Guest na chipsi ni mtaji.Wewe ni tatizo kubwa,huwa ninaangalia sana mitaala ya elimu,wakati mwingine watoto tunawafundisha ujinga.Alisema.
Mhe.Lusinde amesema kuna baadhi ya mambo vijana wanatakiwa kujitathimin na kufanya mambo makubwa na kwa kasi na kuacha kupoteza muda kupoteza fedha kwa kujiunga internet na kuchati kwenye Magroup ya Whatsaap yasiyokuwa na tija kwani ni kupoteza muda na badala yake watumie miundombinu iliyoachwa na Mwalimu Nyerere katika kuwaletea Maendeleo.
“Lazima kuna baadhi ya vitu unapaswa kugundua na kung’amua,lazima miundombinu tuifanyie kazi katika kutuletea maendeleo,kuna mambo mengine yanahitaji haraka,mtu anakwambia polepole ndio mwendo na wewe unakubali.huna shughuli,huna mshahara lakini una simu tatu unachati group hili hadi lile,wewe ni Poyoyo.Amesema.
Hata hivyo,Mhe.Lusinde amewaasa Vijana kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kupambana na rushwa kwani rushwa hunyonya haki ya mtu.
Aidha,Mhe.Lusinde amewataka vijana kujiandaa mapema pindi wanapotaka kufanya maendeleo na akatolea mfano mwanafunzi anayefaulu vizuri mtihani ni Yule aliyejiandaa mapema katika na kudai kuwa ng’ombe hanenepi siku ya mnada.
Kwa upande wake katibu wa Vijana mkoa wa Dodoma Joel Makwaia amesema Mwl.Nyerere alikuwa kiongozi Mzalendo wa Taifa na alijitolea kwa hali na mali ili kuhakikisha taifa linasonga mbele.
Social Plugin