Mwenyekiti wa kamati ya maafa mkoa wa Kagera ambaye pia katibu Tawala mkoa Kagera Profesa Faustin Kamuzora
Na Lydia Lugakila - Malunde 1 blog
Wananchi mkoani Kagera wameshauriwa kujenga majengo yaliyo imara kwa kufuata taratibu zote za ujenzi ili kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza.
Kauli hiyo imetolewa leo Oktoba 13, 2019 na Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya mkoa wa Kagera ambaye pia ni katibu Tawala mkoa wa Kagera Prof. Faustin Kamuzora wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake ikiwa leo ni Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Maafa Duniani.
"Sisi kama mkoa tunatumia siku hii kuwataka wananchi kujiepusha na maafa mbali mbali na pia Halmashauri ziboreshe sheria ya majengo imara ili kujikinga na madhara", alisema Kamuzora.
Amesema wananchi kabla ya kujenga watafute sehemu sahihi kwa kujiepusha kujenga sehemu za mabondeni.
Profesa Kamuzora amesema kutokana na madhara makubwa ambayo yamekuwa yakiukumba mkoa wa Kagera ikiwemo tukio la Septemba 2016 la tetemeko la Ardhi lenye mkubwa 5.9 katika vipimo vya Richter na mengine mengi wananchi wanapaswa kutumia siku hii kujenga majengo yaliyo imara kwa kufuata taratibu zote za ujenzi ili kuepuka na maafa ambayo yamekuwa yakijitokeza.
Amesema mkoa wa Kagera umechukua hatua endelevu kupunguza uharibifu wa maafa katika miundo mbinu na kuendelea kuelimisha wananchi kujenga majengo imara na kufuata taratibu za ujenzi.
Aidha amezitaka Halmashauri za mkoa huo kusafisha mifereji kila wakati ili kuruhusu Maji kupita na kutiririka kuelekea sehemu husika kuepuka mafuriko yanayoweza kuleta maafa.
Hata hivyo amesema mkoa wa Kagera kwa kushirikiana na wadau mbalimbali watahakikisha wanatoa elimu zaidi kwa wananchi ili waweze kupambana na maafa.
Social Plugin