Na Munir Shemweta, WANMM MAFIA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameitaka halmashauri ya wilaya ya Mafia mkoa wa Pwani kuandaa mazingira kupokea uwekezaji wa utalii kwa kupanga na kupima maeneo yake kwa lengo la kuhamasisha wawekezaji wa sekta ya utalii.
Dkt Mabula alisema hayo jana kwa nyakati tofauti aliposikiliza kero za migogoro ya ardhi kwa wananchi wa kata za Baleni na Kilindoni wilayani Mafia mkoa wa Pawani wakati wa ziara yake ya siku mbili kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi, kukagua masijala ya ardhi pamoja na mfumo wa ukusanyaji kodi ya ardhi kwa njia ya kielektroniki.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, eneo la Mafia limekaa kimkakati na yasipofanyika maandalizi mapema kama vile kupima maeneo ya uwekezaji basi migogoro ya ardhi haitaisha na hivyo kuwafanya wawekezaji kushindwa kuwekeza katika wilaya hiyo.
Ameitaka halmashauri ya wilaya ya Mafia kukusaidia kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi katika maeneo ya vijiji na kubainisha kuwa mpango huo unaweza pia kugharimiwa na vijiji husika kwa kuwa gharama yake haizidi shilingi milioni saba kwa kila kijiji na mpango huo utawezesha kuandaliwa maeneo ya kilimo, ufugaji na uwekezaji.
‘’Huu ni mwaka wa uwekezaji Wizara ya Ardhi ni wizara wezeshi tutafanya kila jitihada kupima viwanja katika eneeo la mafia na Kila anayetaka kuwekeza anataka Mafia lakini Mafia yenyewe haijawa tayari alisema Dkt Mabula
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, wizara yake iko tayari kuleta timu maalum ya wapimaji kutoka Wizarani kwa ajili ya zoezi la kupima maeneo mbalimbali katika wilaya hiyo pale ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mafia atakuwa tayari kugharimia fedha ya kujikimu kwa watumishi watakaofanya kazi hiyo.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ardhi alibainisha kuwa, halmashauri ya Wilaya ya Mafia inaweza pia kuandika Andiko litakalowezesha halmashauri hiyo kupata mkopo kwa ajili ya zoezi la upimaji katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Awali baadhi ya wananchi wa Mafia wamelalamikia halmashauri ya Mafia kwa kushindwa kupima maeneo mengi ya wilaya hiyo jambo walilolieleza limechangia kuwepo migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo. Hata hivyo changamoto kubwa inayoikabili wilaya ya Mafia ni kuwa na Mtumishi mmoja wa sekta ya Ardhi.
Maulid Mjenga alimueleza Dkt Mabula kuwa tatizo la upimaji katika wilaya hiyo mbali na mambo mengine lakini limesababisha mipaka ya Shule ya Msingi Kilindoni kutofahamika jambo lililochangia mfadhili aliyejitokeza kujenga ukuta wa shule kushindwa kufanya hivyo kutokana na kutojulikana kwa mipaka ya shule.
Migogoro mikubwa ya ardhi aliyokumbana nayo Dkt Mabula katika ziara yake wilayani Mafia ni pamoja na mgogoro wa wananchi wenye maeneo na kampuni ya Bronkhorst International Contractors Limited unaohusu fidia eneo la Ras Kisimani Mafia, mgogoro wa fidia kati ya kampuni ya Kinasi Lodge na familia ya Mwanahafsa na Bi Lawiya eneo la Utende pamoja pamoja na ule wa fidia katika shamba la Utumaini.
Social Plugin