Na Rajabu Athumani, Mwananchi
Mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Tanga zimezidi kusababisha maafa baada ya vifo vingine vitatu kuripotiwa na kufanya idadi ya waliokufa kufikia 14 hadi leo Jumapili Oktoba 27, 2019 saa 5 asubuhi.
Polisi wamethibitisha kupatikana mwili mmoja katika kitongoji cha bwawani kata ya Sindeni, na miili ya watoto wawili iliyokutwa mtaa wa Wandama kata ya Kwenjugo wilayani Handeni.
Jana mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe alisema watu 10 wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutumbukia kwenye maji kutokana na barabara kukatika, mwingine kusombwa na maji.
Akizungumza leo mkurugenzi mtendaji halmashauri ya wilaya Handeni, William Makufwe amesema miili iliyopatikana ni mitatu.
Joan Luvena, ofisa habari wa Jeshi la Uokoaji na Zimamoto wilayani Handeni amesema juzi watu 51 walilala juu ya mti katika mtaa wa Kwamaraha kutokana na makazi yao kuzingirwa na maji.
Miili hiyo imehifadhiwa katika Hospitali ya Handeni.
Chanzo - MWANANCHI