Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MALIPO YA WAKULIMA WA PAMBA SIMIYU KUFANYIKA KIELEKTRONIKI

Na Stella Kalinga, Simiyu RS

Malipo ya Wakulima wa zao la Pamba Mkoani Simiyu, katika msimu ujao yanatarajiwa kufanyika kwa mfumo wa kielektroniki kupitia huduma ya T-PESA ya Shirika la Mawasiliano Tanzania(TTCL).

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka katika Mkutano wa Wadau wa Pamba uliowahusisha viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali, wataalam wa kilimo, viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS), kwa lengo la kujadili  juu ya malipo ya wakulima wa zao hilo kupitia huduma ya T-PESA uliofanyika Oktoba 02, 2019  mjini Bariadi.

Mtaka amesema kuwa sambamba na mfumo wa ulipaji wa fedha za wakulima wa pamba kwa njia ya Kielekroniki taarifa zote za kilimo zitapatikana kwa njia hiyo huku akiongeza kuwa mfumo huo utasaidia kuondokana na hasara katika vyama vya msingi vya ushirika(AMCOS) iliyokuwa inasababishwa na baadhi ya viongozi wasio waaminifu.

“Tumewaleta hapa TTCL tunataka tufanye digital farming(kilimo kidigitali) malipo ya pamba, mambo yote ya pamba na kilimo kwa ujumla yawe kwenye kiganja chako kwa sababu leo hakuna nyumba ambayo haina simu; ni vizuri elimu hii viongozi wa AMCOS muifikishe kwa wakulima ili wawe  na uelewa wa pamoja,” alisema Mtaka.

Akizungumza katika Mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano  Tanzania  (TTCL) Waziri Kinamba amesema mfumo  huo mpya utaanza kutumika katika msimu ujao na utawasaidia wakulima kupata fedha zao kwa usalama, urahisi, kwa wakati na kupunguza matumizi yasiyofaa.

“Lengo letu ni kutoa suluhu ya matatizo mbalimbali yanayojitokeza katika vyama vya msingi vya ushirika kama upotevu wa fedha, uporaji na tunaamini wakulima wakipata pesa zao kidigitali itaondoa changamoto hizo na kuwafanya wakulima kuwa na maisha bora kutokana na uchumi utakaoboreka baada ya mauzo watakayofanya kupitia TTCL PESA,” alisema Kindamba.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Ushirika Mkoa (SIMCU), Emmanuel Mwelele amesema  kuwa mfumo huu ni mzuri na unalenga kwasaidia wakulima kupata fedha zao kwa usalama na akaahidi kuwa viongozi wa chama hicho watatoa elimu kwa vyama vya msingi vya ushirika(AMCOS) ili wakulima wote wawe na uelewa wa pamoja.

Hadi sasa mkoa wa Simiyu una wakulima wa pamba wapatao 314,000 na matarajio ya uzalishaji katika msimu wa mwaka huu yalikuwa ni  kilo milioni 180, ambapo hadi sasa jumla ya kilo milioni 148 zimekusanywa kutoka kwa wakulima kupitia vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS).

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com