Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JAMAA AFYEKA SHAMBA LA MAHINDI KWA WIVU WA MAPENZI


Picha haihusiani na habari hapa chini

 Ramadhani Bushemeli, ametozwa faini ya Sh300,000 na Serikali ya kijiji baada ya kufyeka shamba la Dotto Magilima akimtuhumu kuwa na uhusiano wa mapenzi na mkewe.


Mkazi huyo wa kijiji cha Nyamigana kata ya Kagu wilayani Geita anadaiwa kufanya kitendo hicho jana Jumatano Oktoba 9, 2019 baada ya kufyeka mahindi na nyanya chungu ikiwa ni baada ya kufika katika shamba hilo na kumkosa Magilima.

Mtendaji wa kijiji hicho, Mugwe Sabuni amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema Ramadhani amekiri kutenda kosa hilo kinyume na sheria.

Mugwe amesema ametozwa faini ya Sh300,000 ambayo amepatiwa Magilima.

Ramadhani akizungumza na waandishi wa habari amesema upendo kwa mkewe ndio chanzo cha kufanya tukio hilo.

“Mimi sijamuona akizini na mke wangu lakini niliambiwa na watu kuwa ana uhusiano naye, hapo ndio hasira zikanishika nikaenda shambani kwake na kufyeka mazao yake,” amesema Ramadhani

Sophia Marko, mke wa Ramadhan amesema aligombana na mumewe na kurudi kwao lakini baadaye alimfuata na kurejea nyumbani lakini walipofika alianza kumlazimisha kuwa ana uhusiano na Magilima.

Naye Magilima amesema asubuhi alikuta shamba lake limefyekwa na alikwenda kutoa taarifa katika uongozi wa kijiji na majirani kumpa taarifa za sababu ya uharibifu huo.

Na Rehema Matowo, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com